Wahajiri haramu 148 waokolewa katika pwani ya Libya
Gadi ya ulinzi wa pwani ya Libya imefanikiwa kuwaokoa wahajiri haramu 148 waliokuwa hatarini kuzama katika maji ya pwani ya nchi hiyo.
Toleo la jana Jumapili la gazeti la Libyan Express limeripoti kuwa, kikosi cha wanamaji cha serikali ya mwafaka wa kitaifa kimetangaza kuwa, askari wa gadi ya ulinzi wa pwani ya nchi hiyo wamefanikiwa katika operesheni tatu tofauti, kuwaokoa wahajiri 148 waliokuwa wakisafirishwa na wafanya magendo ya watu kuelekea Ulaya. Wahajiri hao waliokolewa katika sehemu kadhaa za maji ya Bahari ya Mediterania wakiwa hatarini kuzama.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kikosi hicho cha wanamaji, wahajiri hao haramu wakiwemo wanawake 15 na watoto 11, wengi wao wanatoka Morocco, Algeria, Misri, Somalia na nchi zingine kadhaa za Kiafrika.
Libya ni moja ya vivuko muhimu zaidi vinavyotumiwa na wahajiri haramu wa Kiafrika, ambao kutokana na hali mbaya ya uchumi na usalama katika nchi zao au vita na ukame huamua kuhatarisha maisha yao kwa kuzihama nchi zao na kuelekea Ulaya kutafuta maisha bora kwa kutumia usafiri hatarishi wa baharini.
Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), katika mwaka uliopita wa 2018, zaidi ya wahajiri haramu elfu mbili walipoteza maisha katika bahari ya mediterania.../