Chama kikuu cha upinzani Afrika Kusini chaahidi 'serikali ya ukweli'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5680-chama_kikuu_cha_upinzani_afrika_kusini_chaahidi_'serikali_ya_ukweli'
Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Muungano wa Kidemokrasia (DA) kimezindua ilani yake ya uchaguzi katika jiji la Johannesburg, kitovu cha uchumi na moja ya maeneo kiliyokusudia kuyanyakua kutoka mikononi mwa chama tawala cha ANC katika uchaguzi wa mabaraza ya miji utakaofanyika mwezi Agosti.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Apr 24, 2016 02:49 UTC
  • Chama kikuu cha upinzani Afrika Kusini chaahidi 'serikali ya ukweli'

Chama kikuu cha upinzani nchini Afrika Kusini cha Muungano wa Kidemokrasia (DA) kimezindua ilani yake ya uchaguzi katika jiji la Johannesburg, kitovu cha uchumi na moja ya maeneo kiliyokusudia kuyanyakua kutoka mikononi mwa chama tawala cha ANC katika uchaguzi wa mabaraza ya miji utakaofanyika mwezi Agosti.

Chama hicho ambacho kinaongoza moja ya majimbo tisa ya Afrika Kusini kimepunguza nguvu ya wingi mutlaki wa chama tawala baada ya kuongeza asilimia ya kura zake kutoka asilimia 16 za uchaguzi mkuu wa mwaka 2014 hadi asilimia 22.

Akihutubia wafuasi zaidi ya elfu 20 wa chama hicho katika uwanja wa michezo wa Rand, kiongozi wa DA Mmusi Maimane ameahidi kuunda kile alichosema serikali ya ukweli itakayoandaa ajira na utoaji huduma. "Ni kura ya maamuzi kwa mustakabali wa nchi yetu", alisema Maimane jana Jumamosi akiashiria uchaguzi huo utakaofanyika Agosti 3 mwaka huu.

Mmusi Maimane, mwenye umri wa miaka 35 ambaye mwaka uliopita alikuwa Mwafrika Kusini wa kwanza mweusi kuchaguliwa kukiongoza chama cha Muungano wa Kidemokrasia, amesema ANC inaongoza kama kwamba maisha ya watu weusi hayana umuhimu.

"Tumeona ongezekeo la ufisadi kuanzia katika uongozi wa juu kabisa. Tuna rais aliyepatikana na hatia na Mahakama ya Katiba ya kuvunja Katiba na sheria" alisisitiza Maimane.

Uchaguzi wa Agosti unatazamiwa kushuhudia mchuano mkali katika kipindi cha miaka 22 tangu kusambaratika mfumo wa ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini kutokana na kuongezeka manung'uniko ya wananchi yaliyosababishwa na ufisadi serikalini na kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira.../