Raia 3 wa Somalia 'watoweka' kufuatia shambulizi la anga la Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56868-raia_3_wa_somalia_'watoweka'_kufuatia_shambulizi_la_anga_la_marekani
Kwa akali raia watatu wanahofiwa kuuawa katika shambulizi la anga lililofanywa na ndege isiyo na rubani 'drone' ya Marekani katika eneo la Puntland, kaskazini mashariki mwa Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 26, 2019 08:27 UTC
  • Raia 3 wa Somalia 'watoweka' kufuatia shambulizi la anga la Marekani

Kwa akali raia watatu wanahofiwa kuuawa katika shambulizi la anga lililofanywa na ndege isiyo na rubani 'drone' ya Marekani katika eneo la Puntland, kaskazini mashariki mwa Somalia.

Wakazi wa eneo hilo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia wamesema hatima ya raia watatu wa kijiji cha Ameyra wilayani Iskushuban haijulikani baada ya drone ya Marekani kuvurumisha makombora manne dhidi ya eneo lenye milima mingi la Golis.

Hata hivyo Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani Afrika (Africom) imedai kuwa imeua magaidi watatu kwenye hujuma hiyo ya anga ya jana Ijumaa, viungani mwa wilaya ya  Iskushuban, yapata kilomita 150 kutoka Bosaso, mji mkuu wa kibiashara wa eneo la Puntland.

Mapema mwezi huu, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitangaza kuwa, jeshi la Marekani limeua raia kadhaa wasio na hatia katika moja ya mashambulizi yake ya anga nchini Somalia.

Ramani ya eneo la Puntland, Somalia

Uchunguzi wa Amnesty International ulibaini kuwa, watatu hao walikuwa wakulima ambao hawakuwa na mfungamano wowote na magenge ya kigaidi.

Mwishoni mwa mwaka jana, utafiti uliofanywa na Taasisi ya Hiraal yenye makao makuu yake mjini Mogadishu ulibainisha kuwa, mashambulizi ya anga yanayofanywa kila uchao na Marekani nchini Somalia yameshindwa kulitokomeza au hata kulidhoofisha kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab na badala yake yamekuwa na taathira hasi kwa raia wa kawaida.