Oct 29, 2019 06:52 UTC
  • Watu 16 wauawa katika shambulizi la kigaidi Burkina Faso

Maafisa wa serikali ya Burkina Faso wametangaza kuwa, watu 16 wameuawa katika kile kinachosadikika kuwa ni shambulizi la kigaidi kaskazini mwa nchi.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, watu waliobeba silaha jana Jumatatu waliwashambulia wanakijiji katika eneo la Pobe-Mengao, yapata kilomita 200 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou na kutekeleza ukatili huo.

Mashuhuda wanasema, waliotekeleza jinai hiyo walikuwa wanawalazimisha wanakijiji kuwasaidia kununua silaha, na kila aliyekataa ombi hilo alipigwa risasi na kuuawa papo hapo.

Serikali haijatoa taarifa rasmi kuhusu shambulizi hilo la umwagaji damu za raia wasio na hatia. Ingawaje hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo, lakini magenge yenye mfungamano na makundi ya kigaidi ya al-Qaeda na ISIS yamekuwa yakitekeleza ukatili wa aina hii nchini Burkina Faso na katika nchi jirani ya Mali.

Haya yanajiri chini ya wiki mbili baada ya watu 15 kuuawa baada ya watu waliobeba silaha kushambulia msikiti mmoja kaskazini mwa Burkina Faso. Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, shambulizi hilo lilitokea wakati wa Sala ya Ijumaa katika kijiji cha Salmossi eneo la Oudalan, mpakani mwa nchi hiyo na Mali.

Wanachama wa genge la kigaidi Burkina Faso

Aidha mapema mwezi uliopita, watu 30 waliuawa katika mashambulizi mawili tofauti ya kigaidi yaliyotekelezwa nchini humo katika mkoa wa Sanmatenga nchini humo.

Tangu mwaka 2015 hadi hivi sasa, magenge ya kigaidi yameongeza mashambulizi yao katika maeneo mbalimbali hasa ya kaskazini na mashariki mwa Burkina Faso. Hadi hivi sasa watu wasiopungua 570 wameshauawa kwenye mashambulio hayo.

Tags