Machar: Nisilaumiwe, serikali ya Juba imenizuia kuingia nchini, yumkini nitasafiri Jumatatu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i5701-machar_nisilaumiwe_serikali_ya_juba_imenizuia_kuingia_nchini_yumkini_nitasafiri_jumatatu
Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar amesema binafsi anatamani kusafiri kwenda mji mkuu wa nchi hiyo Juba lakini serikali ya Rais Salva Kiir ndio imemnyima kibali cha kuingia mjini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2016 03:00 UTC
  • Machar: Nisilaumiwe, serikali ya Juba imenizuia kuingia nchini, yumkini nitasafiri Jumatatu

Kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini Riek Machar amesema binafsi anatamani kusafiri kwenda mji mkuu wa nchi hiyo Juba lakini serikali ya Rais Salva Kiir ndio imemnyima kibali cha kuingia mjini humo.

Akiongea na waandishi wa habari katika uwanja mmoja wa ndege mjini Gambella nchini Ethiopia karibu na mpaka wa Sudan Kusini hapo jana, Machar alisema: "Nimeghadhibishwa sana na serikali kwa kunikataza nisisafiri kwenda Juba licha ya zoezi la kuchunguza na kupekua silaha zetu kumalizika."

Machar amesema mpaka sasa yuko kwenye kiza hajui mapokezi atakayoyapata Juba huku akisisitiza kuwa, yumkini akasafiri kesho Jumatatu kuelekea katika mji huo mkuu wa Sudan Kusini.

Madola makubwa ya Magharibi yalikuwa yamemtaka Riek Machar hadi mwishoni mwa jana Jumamosi awe amewasili katika mji mkuu wa Sudan Kusini. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amemtaka Machar kurejea Juba bila ya masharti yoyote kwa mujibu wa mapatano ya amani ya pande hasimu nchini Sudan Kusini, kwa ajili ya kuijenga upya nchi baada ya uharibifu uliosababishwa na mapigano ya ndani nchini humo.

Rieck Machar alitarajiwa kuelekea mji mkuu wa Sudan Kusini, Juba tangu Aprili 18 na kushirikiana na Rais Salva Kiir katika serikali ya umoja wa kitaifa kama Makamu wa Rais wa nchi hiyo.

Awali, serikali ya Sudan Kusini ilidai kuwa imemzuia Machar kurejea nchini kwa kuwa anataka kuingiza silaha na askari zaidi, mbali na wale wapatao ya 1,370 ambao tayari wako Juba.