Wakimbizi laki moja wakwama kambini kwa mafuriko Nigeria
Wakimbizi wa Ndani (IDPs) zaidi ya laki moja wameshindwa kutoka makambini kutokana na mafuriko makubwa yaliyolikumba jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Zainab Gimba, Mbunge wa jimbo hilo amenukuliwa na shirika la habari la Xinhua akisema kuwa, wakimbizi wa ndani katika eneo la Kalabalge jimboni Borno karibu na mpaka wa nchi hiyo na Cameroon wamekwama ndani ya kambi zao kutokana na mafuriko makubwa yaliyoshadidishwa na Mto Kaalia ulioko Cameroon kuvunja kingo zake.
Amesema maelfu ya wanawake na watoto kwenye kambi hizo wameshindwa kufikiwa na misaada ya dharura kama vile chakula na dawa, kutokana na mafuriko hayo yaliyoharibu pia miundimsingi ya eneo hilo.
Mbunge huyo amesema mji wa Rann katika jimbo la Borno halifikiki kutokana na barabara zinazoingia na kutoka kwenye mji huo kufurika, huku hektari 4,000 za mashamba ya kilimo zikiharibiwa na mafuriko hayo.

Hii ni katika hali ambayo, mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini Cameroon na hivyo kusababisha mafuriko yaliyowafanya watu karibu elfu 30 kukosa makazi. Maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua hizo yaliua watu 22 nchini Cameroon hivi karibuni.
Jirani na Nigeria, mafuriko yaliyoyaathiri maeneo ya kusini mashariki mwa Niger tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba hadi sasa yamesaabisha watu zaidi ya elfu 23 kukosa makazi. Aidha watu 57 wameaga dunia katika mafuriko hayo.