Idadi ya waliouawa katika shambulizi la ADF nchini DRC yafika watu 15
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57317-idadi_ya_waliouawa_katika_shambulizi_la_adf_nchini_drc_yafika_watu_15
Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la kuvizia la kundi la wanamgambo wa ADF usiku wa kuamkia jana Jumamosi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeongezeka na kufikia watu 15.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 17, 2019 04:12 UTC
  • Idadi ya waliouawa katika shambulizi la ADF nchini DRC yafika watu 15

Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la kuvizia la kundi la wanamgambo wa ADF usiku wa kuamkia jana Jumamosi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeongezeka na kufikia watu 15.

Maafisa wa serikali katika eneo hilo wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, genge hilo lilitekeleza shambulizi hilo dhidi ya raia, kama jibu na ulipizaji kisasi kwa operesheni ya maafisa usalama ambayo imeua wanachama wa wanamgambo hao zaidi ya 40 ndani ya wiki moja iliyopita.

Miongoni mwa waliouawa katika hujuma hiyo dhidi ya kijiji cha Mbau, katika mji wa mashariki wa Beni, ulioko katika mkoa wa Kivu Kaskazini ni baba na watoto wake watano.

Shambulizi hilo la Ijumaa usiku la magaidi wa ADF lilifanyika siku chache baada ya vikosi vya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutangaza habari ya kuwaangamiza wapiganaji 25 wa kundi hilo la wanamgambo katika mji wa mashariki wa Beni.

Askari wa jeshi la DRC katika mkoa wa Kivu Kaskazini

Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo hao wa ADF ambao asili yao ni Uganda wamekuwa wakiwashambulia raia, maafisa usalama na hata maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi.

Mamia ya Wakongomani wameuawa katika mashambulizi ya wanamgambo wa ADF hususan katika maeneo ya mashariki mwa nchi, tokeo mwaka 2014.