Apr 25, 2016 04:04 UTC
  • Machafuko mashariki mwa DRC kikwazo kwa misaada ya maelfu ya watu

Ofisi ya uratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imesema kuwa, hali mbaya na machafuko huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni kikwazo kikuu cha kuwafikishia misaada ya kibinadamu wahitaji.

Mtandao wa habari wa Africa Time umeinukuu ofisi hiyo ya Ocha ikisema hayo na kuongeza kuwa, operesheni za kijeshi za jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo dhidi ya waasi katika sehemu moja inayojulikana kwa jina la Mpati katika eneo la Masisi, yamepelekea watu 45 kuhitajia misaada ya haraka ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo ya Ocha, wakazi wa mashariki mwa Kongo wanahitajia misaada ya kila namna kuanzia ya kiusalama hadi ya vyakula na nguo na mahitaji mengineyo, lakini machafuko yanazorotesha zoezi la kuwafikishia misaada watu hao.

Ofisi hiyo ya kuratibu misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imeongeza kuwa, licha ya kufanya juhudi kubwa lakini imeshindwa kuwafikia baadhi ya wakimbizi ambao wanaishi katika mazingira magumu sana.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limetumbukia kwenye machafuko tangu miaka 20 iliyopita.

Hadi hivi sasa jeshi la serikali na kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa vimeshindwa kulinda usalama katika eneo hilo.

Tags