Mvua, radi na mafuriko yaua watu 10 nchini Tanzania
Watu tisa wa familia mbili wamefariki dunia katika wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza nchini Tanzania, baada ya nyumba zao kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali duniani.
Mvua hiyo iliyoanza kunyesha majira ya asubuhi, imesababisha maafa hayo kwa baadhi ya nyumba ambazo zipo pembezoni mwa mto ambapo pia daraja muhimu limekatika na kukwamisha mawasiliano na usafiri katika maeneo hayo.
Mkuu wa wilaya hiyo, Dakta Emmanuel Kipole, amewataka wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kuondoka na kwenda katika maeneo ya muda ambayo tayari serikali imeyaainisha ili kuepusha madhara zaidi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongella, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, amewataka wakazi wa maeneo hayo kuchukua tahadhari ili kuepusha kupoteza maisha ya wananchi wengine zaidi.

Wakati huo huo, mvua iliyonyesha jana Jumapili wilayani Arumeru jijini Arusha imesababisha kifo cha mtoto mmoja huku wengine sita wakijeruhiwa baada ya kupigwa na radi.
Katika nchi jirani ya Kenya, Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi, kaskazini magharibi mwa nchi John Lonyangapuo amethibitisha kuwa, hadi sasa maporomoko ya udongo yaliyotokea katika eneo hilo yamesababisha vifo vya watu 43 na kwamba shughuli za uokoaji na kusaka miili zaidi zinaendelea.