Wapiganaji wa Haftar watungua drone ya Marekani 'kimakosa'
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57498-wapiganaji_wa_haftar_watungua_drone_ya_marekani_'kimakosa'
Kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Khalifa Haftar limetangaza kuwa lilitungua ndege isiyo na rubani ya Marekani kwa bahati mbaya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 26, 2019 00:45 UTC
  • Wapiganaji wa Haftar watungua drone ya Marekani 'kimakosa'

Kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Khalifa Haftar limetangaza kuwa lilitungua ndege isiyo na rubani ya Marekani kwa bahati mbaya.

Maafisa wa kundi hilo wamesema drone hiyo ya Marekani ilitunguliwa 'kimakosa' ilipokuwa ikiruka katika anga ya Libya wiki iliyopita.

Jeshi la Marekani jana Jumatatu lilikataa kujibu swali la shirika la habari la Associated Press kuhusu kutunguliwa droni yake hiyo katika anga ya Libya.

Siku ya Jumamosi, jeshi hilo la kamanda muasi Khalifa Haftar lilipiga marufuku kupaa ndege katika anga ya Tripoli. Aidha limekiri kuwa lilitungua ndege isiyo na rubani ya Italia siku chache zilizopita.

Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar, kwa miaka kadhaa sasa limeweza kulidhibiti eneo la mashariki ya Libya kwa msaada na uungaji mkono wa Saudi Arabia, Misri, Imarati na baadhi ya nchi za Magharibi.

Droni ya Marekani katika anga ya Libya

Tarehe 4 Aprili mwaka huu Haftar aliwaamuru wapiganaji wake waushambulie mji mkuu Tripoli kwa shabaha ya kuudhibiti, hatua ambayo imelaaniwa na jamii ya kimataifa.

Zaidi ya watu 1,000 wameuawa na wengine wasiopungua 5,700 wamejeruhiwa katika hujuma hizo za wapiganaji wa Haftar.