Mafuriko yaua watu karibu 40 Kongo DR
Kwa akali watu 39 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa.
Maafisa wa serikali ya Kinshasa wamesema mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo kwa siku kadhaa sasa.
Habari zaidi zinasema kuwa, maporomo ya udongo yameshuhudiwa pia karibu na Chuo Kikuu cha Kinshasa kutokana na mafuriko hayo, na kusababisha maafa na hasara.
Mvua kubwa zinazosababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi zimepelekea makumi ya watu kupoteza maisha katika nchi kadhaa Afrika.
Huko nchini Kenya, watu zaidi ya 60 walipoteza maisha siku chache zilizopita kwenye maporomoko ya udongo yaliyotokea katika kaunti ya Pokot Magharibi, kaskazini magharibi mwa nchi.
Aidha juzi Jumatatu watu tisa wa familia mbili walifariki dunia katika wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza nchini Tanzania, baada ya nyumba zao kusombwa na maji kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini humo.
Zaidi ya watu 50 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko nchini Tanzania kufikia sasa.