UN yakanusha kuwatendea maovu wahajiri walioko Libya
Umoja wa Mataifa umekadhibisha ripoti zinazodai kuwa wafanyakazi wa taasisi hiyo ya kimataifa wamewatendea isivyo wahajiri walioko katika kambi za wakimbizi nchini Libya.
Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa, Filippo Grandi amesema katika makala iliyochapishwa leo katika gazeti la The Guardian nchini Uingereza kwamba, madai yanayosema kuwa Umoja wa Mataifa umewatesa kwa njaa wahajiri hao yanaidhalilisha taasisi hiyo.
Grand ameongeza kuwa, wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa huko Libya wanaishi katika hali na mazingira magumu sana na wanahatarisha maisha yao kwa ajili ya kulinda na kushughulikia wahajiri.
Gazeti la Guardia la Uingereza liliripoti jana Alkhamisi kwamba, limepata wanaraka na ushahidi kwamba Kamisheni Kuu ya Wakimbizi ya Umoja wa Mataifa imesitisha operesheni za kutoa chakula katika kituo cha kuhifadhi wahajiri huko Tripoli. Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kwa njia hiyo, kamisheni hiyo inataka kuwalazimisha wahajiri hao waondoke katika kituo hicho.
Wahajiri wa Kiafrika waliowasili Libya wakiwa njiani kuelekea Ulaya wanaishi katika mazingira mabaya na baadhi yao wanashikiliwa na magenge ya magendo ya binadamu na kuuzwa kama bidhaa.

Mwaka jana wa 2018 karibu wahajiri 3,800 ambao walikuwa na lengo la kuelekea nchi za Ulaya waliaga dunia katika bahari ya Mediterania.