Wasiwasi wa UNCHR kuhusu kuenea machafuko mashariki mwa DRC
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR limesema lina wasiwasi mkubwa kuhusu maisha ya raia wakiwemo wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ambako machafuko yanazidi kushika kasi.
Takribani watu 100 wameuawa kwenye jimbo la Beni tangu kuanza kwa operesheni za serikali za kukabiliana na wapiganaji wa kundi la waasi la ADF 30 Oktoba mwaka huu.
UNHCR inasema mamia ya watu ambao wamekuwa wakikimbia mashambulizi na mapigano baina ya jeshi la serikali na ADF wamekuwa wakipata hifadhi kwenye mji wa Beni ambako usalama mdogo na maandamano makubwa yaliyofanyika mapema wiki hii yamesababisha kukatwa kwa huduma za misaada ya kibinadamu.
Duru zinasema shambulio la karibuni katika kijiji nje ya mji wa Beni liliua watu 19 siku ya Jumatano na wafanyakazi wanne wa huduma za Ebola kuripotiwa kuuawa pia siku hiyo hiyo jioni kwenye kambi ya wafanyakazi wa huduma za Ebola mjini Biakato kwenye ofisi ya kuratibu huduma za Ebola ya Mangina.
Katika taarifa siku ya Ijumaa UNHCR imetoa wito wa kurejeshwa usalama haraka kwenye jimbo la Beni ili mashirika ya misaada ya kibinadamu yaweze kuwasaidia watu walioathirika zaidi jimboni hapo yakiwemo mamia ya familia ambazo kwa sasa zinalala makanisani na mashuleni kwa kuhofia usalama wao.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi mji wa Beni ni makaazi ya takribani watu 500,000 na miongoni mwao 275,000 ni wakimbizi wa ndani ya nchi waliofurushwa makwao kutokana na machafuko.
Kufuatia kuendelea machafuko na hali mbaya ya usalama, wengi wamejikuta wamekwama katikati ya makundi ya wapiganaji.