Amnesty International: Uamuzi wa Tanzania katika Mahakama ya Afrika utazidisha ukandamizaji
(last modified Tue, 03 Dec 2019 14:19:08 GMT )
Dec 03, 2019 14:19 UTC
  • Amnesty International: Uamuzi wa Tanzania katika Mahakama ya Afrika utazidisha ukandamizaji

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International, limesema uamuzi wa Tanzania kujitoa katika kifungu kinachowawezesha raia na mashirika yasiyo ya kiserikali kuishtaki serikali katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake katika mji wa Arusha unahatarisha ongezeko la ukandamizaji nchini humo.

Amnesty imesema kujitoa huko kunawanyima watu na mashirika mbalimbali uwezo wa kupata haki zao za kisheria.

Msemaji wa Amnesty barani Afrika, Japhet Biegon amesema kitendo hicho kinayazuia mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kwenda moja kwa moja mahakamani kudai haki zao kwa makosa ya ukiukwaji wa haki za kibinadamu, jambo ambalo ni jaribio la waziwazi la kukwepa wajibu na majukumu.

Taarifa ya shirika la Amnesty International imesema huu ni ushahidi wa ongezeko la uhasama wa serikali ya Tanzania dhidi ya haki za binadamu na watetezi wa haki hizo na uamuzi huo unadhoofisha mamlaka ya Mahakama ya Afrika, ni usaliti wa wazi kwa juhudi za bara la Afrika za kuanzisha mashirika madhubuti na ya kuaminika yanayoweza kudhamini haki na uadilifu.

Amnesty International imesisitiza kuwa Tanzania kama nchi mwenyeji wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu inapaswa kuwa mfano wa kuigwa na kutafakari tena uamuzi wake wa kujiondoa katika kifungu hicho. Vilevle imeitaka serikali ya Tanzania kuimarisha mfumo wake wa mahakama na kuhakikisha kwamba waathirika wa ukiukwaji wa haki za binadamu wanapata haki zao katika ngazi ya taifa.

Rais John Magufuli wa Tanzania

Tanzania inakuwa nchi ya pili kujiondoa katika kifungu kinachowawezesha raia na mashirika yasiyo ya kiserikali kuishtaki serikali katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu baada ya Rwanda.

Katika barua yake kwa Umoja wa Afrika, ambao wanachama wake ndio waanzilishi wa mahakama hiyo, Tanzania ilielezea kuwa inajiondoa kwa kuwa mahakama hiyo imeshindwa kufanyia kazi maombi yake juu ya ruhusa ya watu na mashirika kushtaki serikali katika mahakama hiyo.

Takribani asilimia 40 ya kesi zilizofunguliwa katika mahakama hiyo ni dhidi ya Tanzania.