Iran: Tunatumai mazungumzo na Nigeria yatapelekea kuachiwa Zakzaky
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema ina wingi wa matumaini kuwa mazungumzo kati ya Tehran na Abuja yatakuwa chachu ya kuanza safari ya kuachiwa huru kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema leo Jumapili kuwa, Tehran inatumai kuwa, mazungumzo ya hivi karibuni kati ya Makamu wa Rais wa Iran katika masuala ya Uchumi, Mohammad Nahavandian na Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, ndio mwanzo wa kuanza mchakato wa kuachiwa huru Sheikh Zakzaky.
Amesema wawili hao walikutana siku chache zilizopita pambizoni mwa Mkutano wa Nchi Zinazouza Gesi Kwa Wingi Duniani mjini Malabo nchini Equatorial Guinea, ambapo mbali na kujadiliana kuhusu umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa pande mbili katika uga wa uchumi na matukio ya kieneo na kimataifa, walizungumzia pia kadhia ya kuendelea kuzuiliwa Sheikh Zakzaky.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imekuwa ikishinikiza juu ya kuachiwa huru mwanachuoni huyo wa Kiislamu kupitia mazungumzo ya kidiplomasia na vikao na maafisa wa serikali ya Abuja.
Haya yanajiri siku chache baada ya Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna nchini Nigeria kukubali ombi la gavana wa jimbo hilo la kupelekwa katika jela kuu ya jimbo hilo Sheikh Zakzaky na mkewe.
Hivi sasa Sheikh Zakzaky ambaye alikamatwa na maafisa usalama wa Nigeria Disemba 2015, anashikiliwa sehemu isiyojulikana na kwa mujibu wa taarifa za uhakika, Mkuu huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anasumbuliwa na matatizo mengi ya kiafya.