Iran: Maadui hawawezi kufunga njia ya Sheikh Ibrahim Zakzaky magharibi mwa Afrika
Hujjatul-Islam Wal Muslimina, Ahmad Marvi ambaye anasimamia haramu ya Imam Ridha (as) katika mji wa Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran amesema kuwa maadui hawawezi kufuta fikra na njia ya Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, barani Afrika kwa kuwa fikra zake zinazidi kuchanua siku hadi siku.
Ayatullah Ahmad Marvi ameyasema hayo alipokutana na binti wa Sheikh Ibrahim Zakzaky katika haramu ya Imam Ridha mjini Mash'hhad na kuongeza kwamba juhudi na kujitolea kwa kiongozi huyo wa harakati ya Kiislamu nchini Nigeria katika kuutumikia Uislamuu, ni kivutio kwa jamii. Akibainisha kwamba Sheikh Zakzaky ameleta mabadiliko katika eneo la magharibi mwa Afrika amesema kuwa, msomi huyo mkubwa amefanya kazi kubwa nchini Nigeria ambapo ameweza kulea makumi ya maelfu ya watu na ni kwa ajili hiyo ndio maana maadui wa Uislamu na sheikh huyo wakajawa na kinyongo. Hujjatul-Islam Wal Muslimina, Ahmad Marvi ameongeza kuwa, msingi uliowekwa na mwanazuoni huyo huko magharibi mwa Afrika, ni fikra ya kimapinduzi ambayo haiwezekani kufutwa.
Kiongozi huyo anayesimamia haramu ya Imam Ridha (as) katika mji wa Mash'had nchini Iran ameashiria dhulma na masaibu ambayo anayapitia kwa sasa Sheikh Ibrahim Zakzaky na kusema, mwanaharakati huyo pamoja na familia yake wanakabiliwa na matatizo makubwa, ambapo vijana wake kadhaa wameuawa shahidi huku yeye na mke wake wakiwa katika mazingira mabaya. Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Waislamu wa Shia nchini Nigeria alitiwa mbaroni pamoja na mke wake katika shambulizi la askari wa nchi hiyo tarehe 13 Disemba 2015 katika Husseiniyah ya mji wa Zariya, katika jimbo la Kaduna, kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Katika shambulizi hilo mamia ya Waislamu wakiwemo watoto watatu wa kiongozi huyo waliuawa shahidi.