Mgogoro wa kidiplomasia, Libya yafunga ubalozi wake Misri
Libya imetangaza habari ya kufunga ubalozi wake katika mji mkuu wa Misri Cairo, kutokana na kile kilichotajwa kuwa sababu za kiusalama.
Ubalozi wa Libya mjini Cairo umewataarifu raia wa Libya wanaoishi nchini Misri juu ya kusimamishwa shughuli zote za ubalozi huo kuanzia leo Jumapili (Disemba 15).
Belqasim Abdul Qader Debres, mwanachama wa Baraza Kuu la Libya ambalo liko chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa amekosoa vikali kauli ya Spika wa Misri, Ali Abdul Aal aliyesema kuwa Cairo inaitambua tu serikali inayoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar, yenye makao makuu yake upande wa mashariki mwa Libya kama mamlaka halali katika nchi hiyo.
Ameeleza bayana kuwa, "Kwa bahati mbaya, Misri inataka kutudhibiti kupitia mapinduzi ya kijeshi, lakini katu hatutaruhusu jambo hilo kufanyika."
Oktoba mwaka huu, mtandao wa gazeti la al Rai al Youm ulivinukuu vyombo vya jeshi la Misri vikitangaza kuwa, Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo na kamanda wa 'Jeshi la Taifa la Libya', Jenerali muasi Khalifa Haftar wamefikia mapatano ya kushirikiana kijeshi chini ya upatanishi wa Imarati.
Haya yanajiri wakati huu ambapo wapiganaji wa Haftar wameshadidisha mashambulizi yao viungani mwa mji mkuu Tripoli na katika mji wa Misrata ulioko kaskazini mwa Libya.
Tangu jenerali huyo muasi aanzishe mashambulizi dhidi ya mji wa Tripoli Aprili mwaka huu kwa msaada wa kila upande wa Saudia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na baadhi ya nchi za Magharibi, hadi sasa amesababisha zaidi ya watu 1090 kuuawa na wengine wasiopungua 5700 kujeruhiwa.