Kashfa ya maziwa ghushi ya Ulaya barani Afrika, yafichuliwa
Jumuiya tano za Ulaya na wazalishaji maziwa wa Afrika wamefichua kwamba, viwanda vya maziwa vya Ulaya vinatengeneza maziwa ghushi ya unga yaliyotayarishwa kwa kutumia mafuta ya mawese na kuyauza barani Afrika.
Televisheni ya France 24 imeripoti kuwa, viwanda vya maziwa vya Ulaya vinatenganisha maziwa na samli yake inayotumiwa kutengeneza bidhaa zenye thamani kubwa, kisha zinatumia maziwa yasiyokuwa na samli kutengeneza maziwa ya unga yanayochanganywa na mafuta ya mawese yanayouzwa kwa makusudi barani Afrika.
Ripoti zinasema kuwa, bei ya maziwa ghushi yanayopelekwa katika nchi za magharibi mwa Afrika kutoka Ulaya iko chini zaidi ya maziwa yanayotengenezwa katika nchi hizo kwa asilimia 30.
France 24 imeripoti kuwa, maziwa ghusi yanayotengenezwa Ulaya na kutumwa Afrika yanaonekana kwa wingi katika maduka makubwa ya bidhaa ya nchi za magharibi mwa bara hilo hususan nchini Senegal.
Wataalamu wa maziwa wanasema kuwa, maziwa ya mtindi na mgando na hata maziwa freshi yanayotengenezwa Ulaya na kutumwa Afrika yanachanganywa na mafuta ya mawese.