Machafuko yawafanya Wakongomani karibu laki 7 kuhama makazi yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i57987-machafuko_yawafanya_wakongomani_karibu_laki_7_kuhama_makazi_yao
Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema karibu watu laki saba katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamelazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na kushtadi ghasia na mapigano.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 19, 2019 21:38 UTC
  • Machafuko yawafanya Wakongomani karibu laki 7 kuhama makazi yao

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema karibu watu laki saba katika maeneo ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamelazimika kuhama makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na kushtadi ghasia na mapigano.

Shirika hilo limesema wakazi 687,500 wa mikoa na miji ya mashariki mwa Kongo DR hivi sasa ama wanaishi makambini kama wakimbizi wa ndani (IDPs) au wamepewa makao ya muda na watu wa familia zao.

Kwa mujibu wa Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka maeneo yaliyoathiriwa zaidi na wimbi hilo la wakimbizi wa ndani mashariki mwa DRC ni Masisi, Rutshuru, na Walikale.

Ripoti zinasema kuwa, tokea Januari mwaka huu hadi sasa, madaktari wa shirika hilo wamewatibu watoto 11,220 waliokuwa na utapiamlo, wahanga 2,310 wa dhulma za kingono na majeruhi 1,980. 

Maisha ya kambini mashariki mwa DRC

Hivi karibuni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNCHR) lilisema katika ripoti kuwa, zaidi ya watu milioni 70 duniani wamelazimika kuhama makazi na nchi zao kutokana na vita, mizozo na mateso.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya watu milioni 25 kati yao ni wakimbizi ambao wamevuka mipaka ya kimataifa na hawana uwezo wa kurudi makwao.