Maeneo yanayozungumza Kiingereza Cameroon yapata hadhi maalumu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58026-maeneo_yanayozungumza_kiingereza_cameroon_yapata_hadhi_maalumu
Bunge la Cameroon limeafiki kuwa maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini humo yapewe hadhi maalumu katika hatua inayolenga kutuliza uasi wa wanaotaka kujitenga.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 21, 2019 21:44 UTC
  • Maeneo yanayozungumza Kiingereza Cameroon yapata hadhi maalumu

Bunge la Cameroon limeafiki kuwa maeneo yanayozungumza Kiingereza nchini humo yapewe hadhi maalumu katika hatua inayolenga kutuliza uasi wa wanaotaka kujitenga.

Sheria hiyo ambayo imepitishwa katika kikao maalumu cha bunge imesema maeneo yanayozungumza Kiingereza ya kaskazini-magharibi na kusini-magharibi 'yatafaidika na hadhi maalumu kwa mujibu wa turathi ya lugha na historia'.  Sheria hiyo inasema  shule na mahakama katika eneo hilo zitapa hadhi maalumu. Hata hivyo waasi wanaotaka kujitenga wanasisitiza kuwa hawataki kingine isipokuwa uhuru kamili kutoka Cameroon na kuunda nchi wanayoiita Ambazonia.

Inakadiriwa kuwa takribani watu 3,000 wameuawa Cameroon tokea mwaka 2017 na wengine 530,000 kukimbia makazi yao kufuatia kuanza uasi katika maeneo ya wanaozungumza Kiingereza.

Wazungumzaji wa Kiingereza wanaunda karibu asilimia 20 ya wakazi wote milioni 20 wa Cameroon, nchi ambayo lugha yake rasmi ni Kifaransa. Wazungumzaji hao wa Kiingereza wanalalamika kuwa wananyanyaswa na kutengwa na serikali kuu na wananyimwa haki zao kama raia wa Cameroon hivyo wanaona ni vyema wapiganie kujitenga.