Makumi wauawa katika mapigano ya kudhibiti kambi ya jeshi Somalia
Makumi ya watu wameuawa katika makabiliano makali baina ya askari wa Jeshi la Taifa la Somalia na wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab karibu na mji wa Baidoa, kusini magharibi mwa Somalia.
Shirika rasmi la habari la Somalia limeripoti kuwa, jeshi la nchi hiyo limefanikiwa kuangamiza wanachama 20 wa kundi la kigaidi la al-Shabaab na kujeruhi wengine 30 katika makabiliano hayo ya jana Jumatatu.
Duru za habari zimeripoti kuwa, jeshi la Somalia limefanikiwa kukomboa kambi ya jeshi ya Goofgaduud Burey toka mikononi mwa al-Shabaab baada ya kujiri mapigano hayo karibu na mji wa Baidoa, yapata kilomita 250 kaskazini magharibi mwa mji mkuu Mogadishu.
Hata hivyo genge la ukufurishaji la al-Shabaab limedai kuwa limepata ushindi mkubwa kwenye mapigano hayo, na kwamba limeua wanajeshi 11 wa Somalia akiwemo Naibu Kamanda wa kambi hiyo ya jeshi, mbali na eti kuteka shehena kubwa ya silaha.
Kundi la al-Shabaab lilikuwa likidhibiti maeneo ya katikati na kusini mwa Somalia lakini lilipokonywa maeneo hayo muhimu, ikiwemo miji mikubwa ambayo ilikuwa mikononi mwa wanachama wa genge hilo mwaka 2015, kufuatia operesheni kubwa zilizofanywa na jeshi la Somalia kwa kushirikiana na askari wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika (AMISOM).
Tangu wakati huo kundi hilo limefanya mashambulizi ya kigaidi katika maeneo tofauti ya Somalia na hata katika ardhi ya nchi jirani ambayo yameua na kujeruhi maelfu ya watu wasio na hatia.