Wanamgambo watiifu kwa jenerali muasi Libya wauteka mji wa pwani wa Sirte
Wanamgambo watiifu kwa Jenerali Muasi Khalifa Haftar wameuteka mji wa pwani wa nchi hiyo wa Sirte, huku Uturuki ikiwa tayari imeanza kutuma wanajeshi wake kuisaidia serikali ya Libya yenye makao yake huko Tripoli inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa.
Ahmad al Mesmari Msemaji wa Jenerali Khalifa Haftar ameeleza kuwa mji wa Sirte unaopatikana umbali wa kilomita zisizopungua 450 mashariki mwa mji mkuu Tripoli umetekwa kikamilifu na wapiganaji hao.
Ameongeza kuwa wapiganaji wao wameuteka mji huo baada ya oparesheni iliyodumu kwa masaa matatu pekee.
Inafaa kuashiria hapa kuwa Jenerali Khalifa Haftar anaungwa mkono kwa hali na mali na Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).
Libya imegawanyika katika kambi mbili moja ikiwa na makao yake katika mji wa Tobruk mashariki mwa nchi; na nyingine huko Tripoli mji mkuu wa nchi hiyo yaani serikali inayotambuliwa kimataifa chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Fayez al Sarraj. Hadi sasa serikali hiyo haijatoa taarifa kuhusu kuangukia mikononi mwa wanamgambo wa Khalifa Haftar mji huo wa pwani wa Sirte.