Usitishaji vita watekelezwa Libya huku vikosi vya Haftar vikiituhumu GNA kuwa imeukiuka
Vikosi vitiifu kwa Khalifa Haftar, kiongozi wa kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) vimeituhumu Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya nchi hiyo GNA kuwa imeyakiuka makubaliano hayo.
Kwa mujibu wa kanali ya televisheni ya Al Hadath, kundi la LNA limetangaza kuwa, baada ya kundi hilo kutangaza usitishaji vita wa upande mmoja, wanamgambo wenye mfungamano na serikali ya Muafaka wa Kitaifa wameyakiuka makubaliano hayo katika medani kadhaa za mapigano magharibi mwa nchi hiyo.
Pamoja na hayo, msemaji wa kundi hilo la Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Haftar ametangaza kuwa, licha ya ukiukaji huo wa usitishaji vita kundi lao litaendelea kuheshimu na kuyatekeleza makubaliano hayo.
Hayo yanajiri wakati ripota wa kanali ya televisheni ya Al Hadath akiripoti kuwa, vikosi vya Serikali ya Muafaka wa Kitaifa vimeanzisha mashambulio ya mizingia katika maeneo mawili ya Ain Zara na Az-Zat'aaranah kusini mwa mji mkuu Tripoli.
Jana usiku kamanda wa kundi la LNA, Khalifa Haftar alitangaza kuwa amelikubali pendekezo la marais wa Russia na Uturuki la kutekeleza usitishaji vita nchini Libya kuanzia usiku wa manane wa kuamkia leo.
Pendekezo hilo lilikuwa limekubaliwa tangu awali na Serikali ya Muafaka wa Kitaifa (GNA) inayotambuliwa rasmi kimataifa.
Itakumbukwa kuwa tangu mwezi Aprili mwaka 2019, vikosi vya Khalifa Haftar vinavyosaidiwa na kuungwa mkono na Saudi Arabia na Imarati na ambavyo vinashikilia eneo la mashariki ya Libya vilianzisha hujuma na mashambulio kwa madhumuni ya kuudhibiti mji mkuu wa nchi hiyo Tripoti na kuiangusha Serikali ya Muafaka wa Kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj.
Katika upande mwingine, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, alitangaza mapema jana kuwa, mazungumzo amani ya Libya yatafanyika mjini Berlin, lakini akasisitiza kuwa pande hasimu katika mgogoro wa nchi hiyo zitapaswa kuwa na nafasi muhimu zaidi ya kusaidia kutafuta suluhisho la mgogoro huo.../