Wapiganaji wa Haftar wakiuka mapatano ya usitishahaji vita Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58463-wapiganaji_wa_haftar_wakiuka_mapatano_ya_usitishahaji_vita_libya
Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya (GNU) imewatuhumu wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar kuwa wamekiuka mapatano mapya ya usitishwaji vita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 12, 2020 08:27 UTC
  • Wapiganaji wa Haftar wakiuka mapatano ya usitishahaji vita Libya

Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya (GNU) imewatuhumu wapiganaji wa jenerali muasi Khalifa Haftar kuwa wamekiuka mapatano mapya ya usitishwaji vita.

Kwa mujibu wa taarifa, Idara ya Habari za Kivita ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa Libya imesema wapiganaji wa Haftar wamevurumisha maroketi ambayo yamelenga vituo vya askari wa serikali katika eneo la Salahuddin kusini mwa mji mkuu, Tripoli.

Wapiganaji wa Haftar nao pia wamedai kuwa vikosi vya serikali vimekiuka mapatano ya usitishaji vita.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetoa taarifa na kusema inaunga mkono mchakato wa kisiasa na kongamano la amani Libya ambalo limepangwa kufanyka karibuni nchini humo. Taarifa hiyo imetoa wito wa kufanyika kongamano la kitaifa Libya ndani ya Libya kwa kuzishirikisha pande zote za kisiasa nchini humo.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya imetoa wito kwa nchi tofauti ziunge mkono Mapatano ya Skhirat  na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Libya.

Baada ya kupinduliwa utawala wa Muammar Gaddafi huko Libya mwaka 2011, nchi hiyo ilitumbukia katika vita vya ndani na hivi sasa kuna serikali mbili hasimu, moja ya mashariki na nyingine ya magharibi mwa nchi hiyo ambapo vikosi vya pande hizo mbili vinaendelea kupigana,

Serikali hizo mbili hasimu ziliibuka mwaka 2014 ambapo moja ina makao makuu yake mjini Tobruk, mashariki mwa nchi na inaungwa mkono na Jenerali muasi Khalifa Haftar, na nyingine ni Serikali ya Muafaka wa Kitaifa Libya (GNA) inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj ambayo inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na ambayo inasimamia maeneo ya magharibi mwa nchi hiyo ukiwemo mji mkuu, Tripoli.

Tokea Aprili mwaka jana wakati Haftar alipoanzisha vita dhidi ya mji mkuu Tripoli, watu wasiopungua 1,100 wameuawa, zaidi ya 5700 wamejeruhiwa na zaidi ya 146,000 kuachwa bila makao.