Jenerali Haftar akataa kusaini makubaliano ya amani ya Libya, Moscow
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58508-jenerali_haftar_akataa_kusaini_makubaliano_ya_amani_ya_libya_moscow
Kamanda wa wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya, Khalifa Haftar aliyekuwa Moscow nchini Russia kwa ajili ya kusaini mapatano na viongozi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ameondoka Russia bila ya kusaini hati ya makubaliano ya amani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 14, 2020 04:45 UTC
  • Jenerali Haftar akataa kusaini makubaliano ya amani ya Libya, Moscow

Kamanda wa wapiganaji wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya, Khalifa Haftar aliyekuwa Moscow nchini Russia kwa ajili ya kusaini mapatano na viongozi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya ameondoka Russia bila ya kusaini hati ya makubaliano ya amani.

Habari zinasema sambamba na kufeli mazungumzo ya amani baina ya pande hizo mbili huko Moscow, mapigano yameshika kasi zaidi nchini Libya hususan kusini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli. Jumamosi iliyopita pande hasimu za Libya zilikubaliana kusitisha mapigano na kuafikia kwamba zitatia saini hati ya kusimamisha vita huko Moscow ili kurasimisha makubaliano hayo. 

Mazungumzo ya pande hizo mbili yaliyofanyika jana yakisimamiwa na mawaziri wa mambo ya nje wa Russia na Uturuki yaliendelea kwa muda wa masaa saba. 

Mapigano yameshika kasi zaidi nchini Libya

Vyombo vya habari vinasema mazungumzo hayo yanaonekana kukwama hususan baada ya Jenerali Khalifa Haftar kukataa kutia saini makubaliano ya mwisho ya kusimamisha vita nchini Libya. 

Kwa sasa Libya imegawanyika sehemu mbili za kiutawala, ambapo moja ni inadhibitiwa na serikali ya umoja wa kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli na inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, huku nyingine ikiwa na mako makuu yake mjini Tobruk chini ya usimamizi wa Khalifa Haftar ambayo inaungwa mkono na Saudia, Imarati, Misri na nchi kadhaa za Magharibi ikiwemo Marekani.