Juhudi za kidiplomasia za kurejesha amani na utulivu nchini Libya
Kupanuka wigo wa mgogoro wa Libya kumepelekea kuongezeka juhudi zenye lengo la kuupatia ufumbuzi mzozo wa nchi hiyo kupitia njia za kidiplomasia.
Katika uwanja huo, Marais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki wamezitaka pande zinazovutana nchini Libya kukubaliana na suala la usitishaji mapigano. Hivi sasa pande mbili zimeafiki wito wa usitishaji vita nchini Libya ingawa usitishaji mapigano huo ni wa hatihati na wa kulegalega.
Fayez Mustafa al-Sarraj, Waziri Mkuuu wa Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya, sambamba na kushiria kwamba, kukubaliana na usitishaji vita kunazuia kuendelea kumwagwa bure bilashi damu za wananchi wa nchi hiyo amesema kuwa: Ninatawaka Walibya waweke kando hitilafu zao na wadumishe umoja kwa ajili ya kuelekea katika mkondo wa amani na utulivu.
Mapigano nchini Libya yameshadidi mno katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Vikosi vitiifu kwa jenerali Khalifa Haftar ambavyo vinaungwa mkono na Imarati, Saudi Arabi na Misri, vinataka kuudhibiti mji mkuu Tripoli na hivyo kuiangusha Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa. Katika uwanja huo, uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani yua Libya nao umekuwa na mchango katika kushadidisha vita na mapigano katika nchi hiyo, kiasi kwamba hivi karibuni ndege zisizo na rubani za Imarati zikiwa na lengo la kumuunga mkono Khalifa Haftar ziliushambuliai mji mkuu Tripolii. Kwa akali watu 28 waliuawa katika shambulio hilo na wengine 18 kujeruhiwa.
Hali hiyo iliifanya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa ya Libya iiombe msaada Uturuki ili kukabiliana na mashambulio hayo na kuulinda mji mkuu Tripoli. Katika safari yake huko Ankara, Waziri Mkuu wa Libya Fayez al-Sarraj alikutana na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ambapo sambamba na mambo mengine, pande mbili hizo zilitiliana saini mikataba miwili muhimu. Makubaliano ya kwanza yalihusiana na mamlaka ya baharini ya Uturuki na Libya katika Bahari ya Mediterania. Mkataba wa pilii ulihusiana na kupanua ushirikiano wa kiusalama na kijeshi baina ya pande mbili.
Licha ya kuwa makubaliano hayo yamekabiliwa na malalamiko mengi ambayo yangali yanaongezeka, lakini inaonekana kuwa, baada ya kushadidi vita vya ndani, Waziri Mkuu wa Libya ameomba rasmi vikosi vya Uruki viwepo katika ardhi ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Kutumwa vikosi vya Uturuki nchini Libya na katika upande mwingine kushadidi hatua na uingiliaji wa wazi wa Saudi Arabia na Imarati katika kufanya mashambulio ya mabomu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo hususan katika miji ya Misrata na Sirte, kivitendo Libya imegeuka na kuwa medani ya mivutano na vita baina ya madola ya kigeni.
Mazingira haya yamezifanya asasi za jumuiya za kimataifa likiwemo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa tahadhari. Baraza la Usalama limeeleza wasiwasi wake lilionao wa hatua za kuzusha machafuko nchini Libya na kusisitiza juu ya udharura wa kuheshimiwa marufuku ya silaha iliyowekewa Libya na kusitishwa uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametangaza katika taarifa yake kwamba: Hatua yoyote ile ya kuunga mkono upande miongoni mwa pande hasimu nchini Libya, inachochea zaidi hali ya mambo na wakati huo huo, inazidi kuhatarisha juhudi za kieneo na kimataifa zenye lengo la kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za kisiasa.
Kuendelea mgogoro wa Libya na kupanuka wigo wake, umezifanya nchi za eneo zianzishe juhudi zenye lengo la kusitisha mapigano katika nchi hiyo. Katika uwanja huo, Marais Vladimir Putin wa Russia na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki baada ya mazungumzo yao hivi karibuni walizitaka pande hasimu nchini Libya kuanza kutekeleza usitishaji vita Jumapili iliyopita ya tarehe 12 Januari.
Pande hasimuu nchini Libya nazo zikatangaza kukubaliana na pendekezo hilo ingawa kwa masharti. Hata hivyo baada ya kupita saa 24 tu, kila upande umeutuhumu upande wa pili kwamba, umekiuka usitishaji vita.
Kwa hakkika jamii ya kimataifa ina matumaini kwamba, usitishaji vita huo uwe hatua ya kwanza ya kuelekea katika kuboresha hali ya mambo nchini Libya. Mkutano wa amani ya Libya umepangwa kufanyika mjini Berlin Ujerumani baadaye mwaka huu kwa kuhudhuriwa na pande hasimu nchini Libya pamoja na mataifa mengine; kwani kuendelea mgogoro wa sasa wa nchi hiyo ni hatari kubwa kwa nchi hiyo na majirani zake.
Aidha ukosefu wa usalama nchini Libya umepelekea kuuongezeka harakati za makundi ya kigaidi ambayo yamekuwa yakielekea katika nchi hiyo. Hali hiyo inatishia kushadidi ugaidi kote ulimwenguni. Si hayo tu, bali ukosefu wa usalama nchini Libya umepelekea pia kuongezeka shughuli za magendo ya binadamu, wahajiri haramu na kuigawa nchi hiyo baina ya madola makubwa ya kigeni na hivyo kuhatarisha vyanzo vya utajiri vya nchi hiyo.
Hivi sasa licha ya kuwa, kumeongezeka juhudi za kieneo na kimataifa kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi wa kidiplomasia mgogoro wa Libya, lakini endapo uingiliaji wa kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo utaendelea sambamba makundi mbalimbali ya Libya kuendelea kutaka hisa ya madaraka bila ya kuzingatia hali inayotawala nchini humo, haionekani kama juhudi hizi za kidiplomasia zitakuwa tiba mujarabu na mwarubaini wa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Libya.