UN yafurahishwa na mkutano wa Berlin wa kujadili mgogoro wa Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58553-un_yafurahishwa_na_mkutano_wa_berlin_wa_kujadili_mgogoro_wa_libya
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka jamii nzima ya kimataifa kukiunga mkono kikao cha Berlin, Ujerumani cha kutafuta njia za kuutatua kisiasa mgogoro wa Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 16, 2020 07:55 UTC
  • UN yafurahishwa na mkutano wa Berlin wa kujadili mgogoro wa Libya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameitaka jamii nzima ya kimataifa kukiunga mkono kikao cha Berlin, Ujerumani cha kutafuta njia za kuutatua kisiasa mgogoro wa Libya.

António Guterres amesema hayo leo wakati huu wa kukaribia kufanyika mkutano wa kimataifa wa kujadili mgogoro wa Libya, mjini Berlin, Ujerumani, akisisitiza kuwa, kukomeshwa mapigano, kutekelezwa usimamishaji vita, kupigwa marufuku matumizi ya silaha, kufanyiwa marekebisho mfumo wa kiusalama, kurejea katika mchakato wa kisiasa, kufanyika marekebisho ya kiuchumi na kuheshimiwiwa sheria za haki za binadamu ni ajenda sita kuu zitakazojadiliwa kwenye kikao hicho.

Fayez al Sarraj

 

Katibu Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amezitaka pande hasimu nchini Libya kuheshimu makubaliano ya kusimamisha vita ili kuruhusu kufanyika vizuri kikao cha Berlin na kuongeza kuwa, lengo la kuitishwa kikao hicho ni kuiweka jamii nzima ya kimataifa chini ya mwavuli mmoja kwa ajili ya kukabiliana na mgogoro wa Libya na kurudisha mchakato wa kisiasa katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kupitia mazungumzo baina ya makundi yote ya Libya.

Mkutano wa kuzungumzia mgogoro wa Libya umepangwa kufanyika siku ya Jumapili ya tarehe 19 Januari mjini Belin Ujerumaini. Wawakilishi wa nchi mbalimbali kama vile Ujerumaini, Marekani, Russia, Uingereza, Ufaransa, China, Imarati, Uturuki, Congo Brazzavile, Italia, Misri, Algeria na taasisi nne za kimataifa na za kieneo yaani Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu zitashiriki kwenye mkutano huo.

Fayez al Sarraj, Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa pamoja na jenerali muasi Khalifa Haftar anayeongoza kundi linalojiita "Jeshi la Taifa la Libya" nao watashiriki mkutano huo.

Jenerali muasi, Khalifa Haftar