Waislamu Nigeria waendelea kulalamikia kushikiliwa Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imetoa taarifa ya kulalamikia kuendelea kushikiliwa gerezani kiongozi wa harakati hiyo, Sheikh Ibrahim Zakzaky.
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imesema katika taarifa yake hiyo kwamba, viongozi wa jimbo na wa serikali ya Nigeria ndio wanaopaswa kubeba dhima ya kushikiliwa kinyume cha sheria Sheikh Zakzaky na wasiibebeshe lawama mahakama.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, tarehe pili Disemba 2016 Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa hukumu kwamba kutiwa mbaroni Sheikh Zakzaky na mkewe ni kinyume cha sheria na kunakinzana na katiba ya nchi hiyo.
Hivi karibuni Gavana wa Jimbo la Kaduna nchini Nigeria, Nasir Ahmad el Rufai pamoja na Aisha Dikko, Mwanasheria Mkuu wa jimbo hilo walidai kuwa hatima ya Sheikh Ibarahim Zakzaky na mkewe iko mikononi mwa mahakama na wala haiwahusu viongozi wa jimbo hilo. Hata hivyo Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imepinga vikali madai hayo na kusema kuwa, tayari Mahakama Kuu imeshatoa amri ya kuachiliwa huru kiongozi huyo na mkewe, lakini viongozi wa jimbo la Kaduna na wa serikali wamekataa kutekeleza amri ya mahakama.
Sheikh Ibrahim Zakzaky, (66) na mkewe Malama Zeenat walitiwa nguvuni tarehe 13 Desemba 2015 wakati wanajeshi wa Nigeria walipovamia Hussainia ya Baqiyatullah na nyumba ya mwanazuoni huyo katika mji wa Zaria. Waislamu wasiopungua 1,000, wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky, waliuawa shahidi katika shambulio hilo.
Wanaharakati na wapigania haki katika maeneo mbalimbali ya dunia wanaendelea kuitaka serikali ya Rais Muhamadu Buhari imuachilie huru Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe.