Jan 19, 2020 08:03 UTC
  • Shambulizi la bomu laua na kujeruhi watu 14 nchini Somalia

Mripuko wa bomu uliolenga wafanyakazi wa mradi wa ujenzi wa Kituruki nchini Somalia umeua watu watatu na kujeruhi wengine 11.

Duru za habari zinasema kuwa, gari lililokuwa limesheheni mabomu liliripuka jana Jumamosi nyakati za adhuhuri karibu na mgahawa ambao wakandarasi wa Kituruki hupata chakula katika mji wa Afgoye karibu na mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, shambuizi hilo lilifanyika yapata kilomita 30 nje ya Mogadishu na liliwalenga wakandarasi wa Uturuki wanaojenga barabara kuu ya kuunganisha miji ya Afgoye na Mogadishu.

Awali Balozi wa Uturuki mjini Mogadishu, Mehmet Yilmaz alisema kwamba, kwa mujibu wa taarifa za awali kutoka eneo la tukio, hakuna aliyepoteza maisha lakini kuna majeruhi.

Kundi la al-Shabaab limekuwa likihusika na mashambulio ya mabomu nchini Somalia

Wakandarasi hao wa Kituruki wamekuwa wakiendeleza ujenzi huo wa barabara uliofadhiliwa na Qatar tangu Disemba mwaka jana. Watu karibu 90 wakiwemo Waturuki wawili waliuawa katika shambulizi jingine la bomu katika mji huo wa Afgoye mnamo Disemba 28 mwaka uliomalizika.

Hii ni katika hali ambayo, usiku wa kuamkia jana, vikosi vya jeshi la Somalia vilitangaza kuwa vimefanikiwa kuzima shambulizi la kundi la kigaidi na ukufurishaji la al-Shabaab katika mji huo wa Afgoye karibu na mji mkuu wa nchi hiyo, Mogadishu. 

Tags