Msemaji wa Haftar: Mgogoro wa Libya hauwezi kutatuliwa kisiasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58771-msemaji_wa_haftar_mgogoro_wa_libya_hauwezi_kutatuliwa_kisiasa
Msemaji wa vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya (Libyan National Army) vinavyoongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar amesema kuwa, mgogoro wa nchi hiyo hauwezi kupatiwa ufumbuzi kupitia njia za kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 27, 2020 04:45 UTC
  • Msemaji wa Haftar: Mgogoro wa Libya hauwezi kutatuliwa kisiasa

Msemaji wa vikosi vinavyojiita Jeshi la Taifa la Libya (Libyan National Army) vinavyoongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar amesema kuwa, mgogoro wa nchi hiyo hauwezi kupatiwa ufumbuzi kupitia njia za kisiasa.

Meja Jenerali Ahmed al-Mismari amesisitiza kuwa, utatuzi wa mgogoro wa sasa unaoikabili Libya ni vita na hatua za kijeshi ni siyo mazungumzo na njia za kisiasa.

Msemaji huyo wa Jenerali Khalifa Haftar anasema hayo katika hali ambayo, kumeendelea kushuhudiwa juhudi za kieneo na kimataifa zenye lengo la kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa nchi hiyo.

Hivi karibuni mji mkuu wa Ujerumani Berlin ulikuwa mwenyeji wa mkutano wa kimataifa wa Libya ambapo washiriki wa mkutano huo walisisitiza juu ya kuhitimishwa mapigano nchini humo na kutouunga mkono upande wowote miongoni mwa pande zinazozozana katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Mapigano ya ndani nchini Libya

Libya ilitumbukia katika vita na machafuko ya ndani yaliyochochewa na nchi za kigeni na uingiliaji kati wa madola makubwa kama Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya baada ya kuondolewa madarakani kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi mwaka 2011.   

Hata hivyo mgogoro wa Libya ulizidi kuwa mkubwa baada ya janerali muasi Khalifa Haftar anayeungwa mkono na Saudi Arabia, Imarati na Misri kuanzisha mashambulizi ya pande zote dhidi ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli mwezi Aprili mwaka jana.