Wapiganaji wa Haftar: Uturuki ina askari 3000 nchini Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i58840-wapiganaji_wa_haftar_uturuki_ina_askari_3000_nchini_libya
Msemaji wa vikosi vya kundi la wapiganaji linalojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' amesema kuwa Uturuki imetuma askari 3000 nchini Libya.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jan 30, 2020 13:36 UTC
  • Wapiganaji wa Haftar: Uturuki ina askari 3000 nchini Libya

Msemaji wa vikosi vya kundi la wapiganaji linalojiita 'Jeshi la Kitaifa la Libya' amesema kuwa Uturuki imetuma askari 3000 nchini Libya.

Ahmed Al-Mismari ameyasema hayo leo na kubainisha kwamba Uturuki ilipeleka Libya askari wake kutoka Syria kupitia uwanja wa ndege wa Misrata, Mitiga na bandari ya Tripoli. Aidha msemaji wa wapiganaji wa Jenerali Muasi Khalifa Haftar ameongeza kuwa, serikali ya Uturuki ilituma nchini humo meli mbili za kivita, makombora ya kukabiliana na mashambulizi ya anga na ngao ya makombora kupitia bandari ya mjini Tripoli. Inafaa kuashiria kuwa serikali ya Uturuki inaunga mkono serikali ya Maridhiano ya Kitaifa inayoongozwa na Fayez al-Sarraj na ambayo inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa.

Askari wa Uturuki wanaodaiwa kutumwa Libya

Katika wiki chache zilizopita Uturuki ilitangaza azma yake ya kupeleka askari wa nchi hiyo huko Libya, hata hivyo ilibadili msimamo wake huo baada ya kufanyika mkutano wa mjini Berlin, Ujerumani hapo tarehe 19 ya mwezi huu. Aidha serikali ya Ankara kupitia Mevlüt Çavuşoğlu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki ilitupilia mbali madai ya kutuma askari wake kaskazini mwa Afrika, na badala yake ikasema kuwa ingetuma tu nchini humo washauri wa masuala ya kijeshi. Mashambulizi ya wapiganaji wa Khalifa Haftar kwa lengo la kudhibiti mji wa Tripoli yalianza Aprili mwaka jana na hadi sasa yameibua mgogoro mkubwa ndani ya taifa hilo.