30 wauawa Kongo DR katika shambulizi la wanamgambo wa ADF
Kwa akali watu 30 wameuawa katika shambulizi la wanamgambo wa ADF huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Duru za habari zinaarifu kuwa, vijiji vinne katika mji wa Beni wa mashariki mwa nchi vilishambuliwa na wapiganaji hao ambao asili yao ni Uganda, ambapo raia wasiopungua 30 waliuawa kwa kuchomwa visu na kupigwa mapanga.
Vyanzo vingine vya habari vinasema idadi ya raia waliouawa katika shambulizi hilo la usiku wa kuamkia Jumatano ni 38 na kwamba wengine waliojeruhiwa vibaya wanaendelea kupata huduma za matibabu mjini hapo.
Haya yanajiri siku chache baada ya ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti ya Kongo ya Chuo Kikuu cha New York inayofuatilia mauaji ya raia katika eneo la Kivu tokea mwaka 2017 kusema kuwa, karibu raia 200 wameuawa katika mikoa miwili ya mashariki mwa DRC katika makabiliano baina ya maafisa usalama na magenge ya wanamgambo likiwemo kundi la waasi la ADF la Uganda ndani ya siku 31 za mwezi uliopita wa Disemba 2019.
Katika miezi ya hivi karibuni, wanamgambo hao wa ADF ambao asili yao ni Uganda wamekuwa wakiwashambulia raia, maafisa usalama na hata maafisa wa afya wanaopambana na ugonjwa hatari wa Ebola, mashariki mwa nchi.