Wanamgambo waua watu 62 mashariki mwa DRC
Watu wenye silaha wameripotiwa kuua watu wasiopungua 62 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mlolongo wa mashambulizi yaliyolikumba eneo hilo.
Jeshi la nchi hiyo limesema katika taarifa yake ya jana Jumamosi kwamba wimbi hilo la mashambulizi ya waasi dhidi ya raia limetokea baada ya jeshi la serikali kuanzisha kampeni maalumu ya kupambana na waasi wa ADF wa Uganda ambao wanafanya mashambulizi katika eneo la Beni, la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kundi la haki za binadamu la CEPADHO limesema kuwa, waasi wa ADF wameua raia wasiopungua 74 kwa kutumia visu na bunduki. Wengi wa wahanga hao ni wanawake na watoto wadogo.
Kundi hilo limeongeza kuwa, mauaji hayo yamefanyika katika vijiji vipatavyo 10 kwenye kipindi cha masaa 48 ya hadi ilipotolewa taarifa hiyo. Jeshi la Kongo limekuwa likisisitiza mara kwa mara kwamba limeangamiza waasi hao baada ya kuua makamanda wao wa ngazi za juu na kuteka kambi na maficho yao mengi kwenye misitu mizito iliyoko katika mpaka wa Kongo DR na Uganda.
Hata hivyo waasi hao wa ADF walioingia Kongo kutokea Uganda katika miaka ya 1990 wamekuwa wakifanya mashambulizi mara kwa mara ya kuvamia raia na maeneo yao kwa madai ya kulipiza kisasi operesheni za jeshi la Kongo.
Genge hilo ni moja ya darzeni ya magenge ya waasi yanayoendesha shughuli zao mashariki mwa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa madini.
Kwa makumi ya miaka sasa eneo hilo la Maziwa Makubwa ya Afrika limekuwa na vita visivyoisha ambavyo vimeshasababisha mamilioni ya watu kupoteza maisha. Maafisa wa Kongo wanasema kuwa, watu wasiopungua 30 waliuawa Jumatano usiku karibu na mji wa Oicha huku taasisi za kiraia zikisema kuwa, makumi ya raia wengine waliuawa siku ya Alkhamisi katika vijiji vya karibu na mji huo.