Ramaphosa: Tusiruhusu vita vya niaba barani Afrika
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59056-ramaphosa_tusiruhusu_vita_vya_niaba_barani_afrika
Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika amesema kuwa, Waafrika hawapasi kuruhusu bara lao liwe medani ya vita vinavyopiganwa kwa niaba ya pande nyingine.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Feb 10, 2020 04:04 UTC
  • Cyril Ramaphosa
    Cyril Ramaphosa

Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika amesema kuwa, Waafrika hawapasi kuruhusu bara lao liwe medani ya vita vinavyopiganwa kwa niaba ya pande nyingine.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini aliyasema hayo jana katika mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika mjini Addis Ababa na kuongeza kuwa, Waafrika hawapasi kuwaruhusu wageni kuwasha moto wa vita na mizozo barani mwao na kuzitumbukiza nchi za bara hilo katika vita vya niaba. 

Ramaphosa amesema: Waafrika wote wanawajibika kutengeneza amani na ustawi kwa ajili ya Afrika.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini mbaye jana alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Umoja wa Afrika amezitaka nchi zote za bara hilo kusimama kidete kwa ajili ya kukabiliana na njama zinazotaka kulitumbukiza bara hilo katika mapigano na vita vya ndani.

Mkutano wa viongozi wa Afrika, Addis Ababa

Ramaphosa amekutaja kukomesha machafuko nchini Libya na kukamilisha makubaliano ya amani nchini Sudan Kusini kuwa ndiyo malengo mawili muhimu zaidi ya kipindi chake kama mwenyekiti mpya wa umoja wa Afrika. 

Mkutano wa viongozi wa nchi za Afrika ulianza kazi zake jana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa ukijadali masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na mgogoro wa Libya, mpango wa Donald Trump wa "Muamala wa Karne" kuhusu Palestina na suala la kuondolewa Sudan katika orodha ya magaidi ya Marekani.