UN: Uvamizi wa nzige bado ni tisho kubwa Pembe ya Afrika
(last modified Wed, 26 Feb 2020 07:42:55 GMT )
Feb 26, 2020 07:42 UTC
  • UN: Uvamizi wa nzige bado ni tisho kubwa Pembe ya Afrika

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) limesisitiza kuwa hali ya mlipuko wa nzige wa jangwani bado ni mbaya katika nchi za Pembe ya Afrika na kwamba inahatarisha usalama wa chakula haswa nchini Ethiopia, Somalia na Kenya.

Taarifa ya FAO imetahadahrisha kuwa makundi mpya ya nzige yanatarajiwa kuibuka katika wiki zijazo.

Taarifa zinasema nchini Ethiopia nzige wamekuwa wakitaga mayai yao, na wanakula mioto ya kijani katika msimu huu wa  upanzi. Nchini Kenya makundi ya nzige yameendelea kuripotiwa kwenye maeneo ya kaskazini na katikati, ambapo wengi kati yao wametaga mayai. Nchi za Tanzania na Uganda pia zimeathiriwa na nzige ambao pia wameripoptiwa kuvuka bahari na kuingia Yemen na Saudi Arabia.

FAO imetoa wito wa msaada wa dharura wa kukabiliana na nzige na hadi sasa imepokea  dola milioni 6.5 kutoka mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa na wafadhili wengine wa kimataifa kwa ajili ya operesheni za kutokomeza nzige hao.

Wakulima wakiwa wamezingirwa na nzigo wa jangwani

Mazungumzo yanaendelea ili kupata dola nyingine milioni 10 wakati huu ambapo FAO imeomba dola milioni 138 ikiwa nyongeza kwa takribani asilimia 50 kutoka ombi la mwezi mmoja uliopita.

Fedha hizo zinalenga kusaidia mataifa 8 ya Mashariki mwa Afrika yaliyoathiriwa na nzige ambapo dola milioni 50.5 kati ya hizo ni kwa ajili ya Ethiopia.

Tags