Jeshi la Somalia lapambana na wanamgambo wa Ahlu Sunnah Wal Jama’a (ASWJ)
Jeshi la Somalia mapema leo Ijumaa limepambana na wanamgambo wa kundi moja la kikanda katika kile kinachotajwa na Wasomali kuwa ni mapigano makali zaidi baada ya misuguano ya kisiasa inayoendelea kuikwamisha nchi hiyo katika dimbwi la ghasia na machafuko.
Mivutano ilianza jioni ya jana Alkhamisi baina ya jeshi la taifa la Somalia na wanamgambo wa kundi la Ahlu Sunnah Wal Jama’a (ASWJ) ambao walikuwa na mchango mkubwa katika kupambana na makundi ya kigaidi ya al Qaida na al Shabab.
Mapigano hayo yalianza mapema leo katika mji wa Dhusamareb ambao ni Makalu makuu ya mkoa wa Galmudug na kuenea katika mji wa Guriel ulioko umbali wa kilomita 60 kutoka katika mji huo.
Watu walioshuhudia wanasema, jeshi la taifa la Somalia limeshambulia nyumba moja ambayo ni makazi ya viongozi wa kundi la wanamgambo wa ASWJ na kwamba pande mbili zimeshambulia kwa maroketi na mizinga.
Wakazi wa Dhusamareb wanasema mji huo ulikuwa kama moto wa Jahannamu baada ya miaka 11 ya utuivu na suluhu baina ya kundi hilo la serikali kuu ya Mogadishu.
Wachambuzi wa mambo wanasema mapigano ya ndani nchini Somalia yanakwamisha juhudi za kimataifa za kupambana kundi la kigaidi la al Shabab.
Kundi la kigaidi la al-Shabab lilianzisha hujuma zake nchini Somalia mwaka 2007 na limekuwa likifanya operesheni za kigaidi katika mji mkuu, Mogadishu na maeneo mengine ya Somalia na pia katika nchi jirani ya Kenya. Magaidi hao walitumuliwa Mogadishu Agosti 2011 katika operesheni iliyofanywa na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika, AMISOM, lakini limekuwa likifanya mashamabulizi ya kuvizia mara kwa mara.