Watanzania waendelea kutoa radiamali kufuatia Bernard Membe kupigwa kalamu nyekundu na CCM
Uamuzi wa Kamati Kuu ya chama cha Mapinduzi CCM wa kumfukuza uanachama Bernard Membe kada wa chama hicho na aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, umepokelewa kwa hisia tofauti na Watanzania.
Wakati wengine wakisema uamuzi huo ulikuwa sahihi kulingana na taratibu za chama hicho, lakini baadhi wamekosoa uamuzi tajwa na kubainisha kwamba badala ya kumfukuza, angeweza kuonywa tu kama ilivyowahi kutokea mwaka 2014 ambapo Membe alituhumiwa kwa kuanza kampeni mapema pamoja na wenzake watano na hivyo akaonywa kwa hatua hiyo. Katika uwanja huo Suleiman Mwambipile mkazi wa Mbeya, ametilia shaka uamuzi huo wa CCM kwa kuhoji kuwa, Membe ametenda makosa yake tangu mwaka 2014, lakini kitendo cha CCM kumfukuza uanachama hivi sasa inaweza kuwa ni mtego wao kwa upinzani. “CCM ina mbinu nyingi sana, sitashangaa Membe kuona ametumwa kwa njia ya kufukuzwa ili ahamie chama mojawapo cha upinzani na akapewa mkoba wa kupeperusha bendera ya kiti cha urais uchaguzi ujao, halafu afanye kila linalowezekana kuhakikisha CCM inaibuka kidedea tena.” Amesema.
Naye Zephania Mollel mkazi wa Arusha amesema hatua ya CCM kumfukuza Bernard Membe inaonesha ni jinsi gani chama hicho kinavyokabiliwa na mgogoro wa ndani ambao unaweza kuathiri hata utendaji kazi wa serikali. “Sababu iliyochangia kufukuzwa ni msimamo wake usioyumba wa kutoa maoni namna anavyoona nchi inaongozwa. Mfano suala la kubana matumizi, Membe alikosoa hiyo hatua hadharani baada ya hapo amekuwa anachukuliwa kama adui.” Amesema Mollel. Itakumbukwa kuwa baada ya Membe kufukuzwa na CCM hivi karibuni alinukuliwa akisema kwamba kufukuzwa kwake kumetokana na uamuzi wake wa kutaka kugombea urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu na kwamba anafurahi kwa kuwa huru. “Nafurahi sasa niko huru, nitafanya mambo yangu kwa uhuru bila kuhojiwa na kuulizwaulizwa na mtu yeyote. Si unajua nimefungua kesi mahakamani na hii ni kesi ya kisiasa.”
Aidha aliendelea kusema: “Kuwepo kwangu CCM kulikua kunanifunga kutozungumza baadhi ya mambo, lakini sasa, kwanza nitakuwa na muda mzuri ...” Alisema. Membe alipewa adhabu ya kufukuzwa ndani ya chama kutokana na tuhuma za utovu wa nidhamu zilizokuwa mbele ya Kamati Kuu ya CCM, akishtakiwa pamoja na wenzake wawili ambao ni makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba. Katika uwanja huo Peter John mkazi wa Arusha na ambaye ni mwanachama wa CCM binafsi amesema kuwa, hafahamu sababu iliyotajwa dhidi ya Membe kama ni kweli: “Walisema alifanya makosa hayo hayo ya mwaka 2014 ambayo chama kilimchukulia hatua za kinidhamu.” Amesema.