Dk Bashiru amjibu Membe, asema kama tatizo ni urais tukutane uwanjani
-
Bashiru Ally
Katibu Mkuu wa chama cha Mapinduzi CCM nchini Tanzania, Dk Bashiru Ally amemjibu Bernard Membe aliyekuwa kada wa chama hicho na Waziri wa Mambo ya Nje wa Zamani wa nchi hiyo, akimtaka kugombea urais kwa tiketi ya chama kingine cha siasa ili wakutane uwanjani.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akijibu swali kuhusu kile alichokisema Membe baada ya kuvuliwa uanachama.
Itakumbukwa kuwa wiki iliyopita Membe alinukuliwa akisema kuwa amevuliwa uanachama kutokana na nia yake ya kutaka kupambana na mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Akijibu kauli hiyo Dk Bashiru amesema kuwa katiba ya CCM haisemi kama ukishafukuzwa kwenye chama hauruhusiwi kugombea kwenye chama kingine hivyo Membe aende na nguvu zake pamoja na wafuasi wake tukutane uwanjani. “Ukishafukuzwa kwenye chama cha CCM katiba haisemi huwezi kugombea kwenye vyama 19 vilivyobaki, ila ukifungwa ndio unaweza ukakosa sifa au ukikwepa kodi, adhabu aliyopewa (Membe) haihusu sheria za nchi.” Amesema Katibu Mkuu wa chama cha Mapinduzi CCM.
Membe na makatibu wakuu wawili wastaafu wa chama cha Mapinduzi CCM yaani Abdulrahman Kinana na Yusufu Makamba, walifikishwa mbele ya kamati ndogo ya udhibiti na nidhamu kujibu mashtaka ya kinidhamu dhidi yao. Wanasiasa hao waliingia matatani baada ya sauti zao pamoja na za wanachama wengine watatu kuvuja katika mitandao ya kijamii wakizungumzia kuporomoka kwa chama hicho na uenyekiti wa Magufuli.
Katika mchakato huo iliamuliwa kuwa Makamba atasamehewa makosa yake, Kinana atakuwa chini ya uangalizi kwa miezi 18, kipindi ambacho hataruhusiwa kugombea uongozi, wakati Membe alivuliwa uanachama na hivyo hataweza kutimiza ndoto yake ndani ya chama hicho.