Apr 28, 2016 15:15 UTC
  • Serikali: Mripuko wa kipindupindu umeua watu 45 Zanzibar

Wizara ya Afya ya Zanzibar imesema kwa akali watu 45 wamepoteza maisha kutokana na mripuko wa kipindupindu tangu mwezi uliopita wa Machi hadi sasa.

Muhammad Dahoma, Mkurugenzi wa Kitengo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa ambacho kiko chini ya Wizara ya Afrika visiwani humo amesema watu wapatao 3,000 wamelazwa hospitalini baada ya kuambukizwa ugonjwa huo hatari.

Amesema serikali imeanzisha vituo kadhaa katika visiwa hivyo vya Unguja na Pemba ili kuwatenga walioambukizwa ugonjwa huo sambamba na kupiga marufuku uuzaji wa vyakula na vinywaji katika vibanda na maeneo ya wazi.

Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha visiwani Zanzibar na kuziba kwa mabomba ya kupitisha majitaka ni miongoni mwa sababu ziliotajwa kusababisha kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu visiwani humo.

Mripuko huo wa kipindupindu unatishia sekta ya utalii haswa ikizingatiwa kuwa watalii wengi huvitembelea visiwa hivyo kuanzia mwezi Juni.

Wimbi jipya la maambukizi ya ugonjwa wa kipindupindu ambalo lilianzia katika kambi ya wakimbizi wa Kisomali huko mashariki mwa Kenya sasa limeenea zaidi katika nchi kadhaa za Afrika.

Maafisa wa serikali ya Zambia wamesema watu wasiopungua 16 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa kipindupindu tangu kuanza ugonjwa huo mjini Lusaka mwezi Februari mwaka huu, huku kesi 734 za maambukizi zikiripotiwa katika mji huo mkuu wa nchi hiyo.

Tags