Corona yaingia Rwanda, virusi hivyo vyasababisha shule kufungwa Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59764-corona_yaingia_rwanda_virusi_hivyo_vyasababisha_shule_kufungwa_kenya
Serikali ya Rwanda imethibitisha kuwa na mgonjwa mmoja aliyeambukizwa virusi vya Corona, huku ugonjwa huo ukiendelea kuenea kwa kasi katika nchi za Afrika na kote duniani kwa ujumla.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 15, 2020 15:44 UTC
  • Corona yaingia Rwanda, virusi hivyo vyasababisha shule kufungwa Kenya

Serikali ya Rwanda imethibitisha kuwa na mgonjwa mmoja aliyeambukizwa virusi vya Corona, huku ugonjwa huo ukiendelea kuenea kwa kasi katika nchi za Afrika na kote duniani kwa ujumla.

Mgonjwa huyo raia wa India aliingia katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki Jumapili iliyopita akitokea mjini Mumbai, na hivi sasa yupo chini ya karantini.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Rwanda, mgonjwa huyo hakuwa na dalili zozote za ugonjwa wa Corona alipowasili nchini humo, lakini baada ya siku tano, alipatwa na homa kali na kuamua kwenda katika kituo cha afya kwa ajili ya matibabu, na ndipo vipimo vikaonyesha kuwa amekubwa na virusi hivyo vya Covid-19.

Huku hayo yakiarifiwa, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amethibitisha kesi mbili mpya za ugonjwa wa Corona nchini humo, na kuongeza kuwa watu 22 waliowasiliana na mgonjwa wa kwanza wa virusi hivyo anayeendelea kutibiwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, wamewekwa karantini. 

Akihutubia taifa leo Jumapili jijini Nairobi, Rais Kenyatta ameagiza kufungwa kwa shule zote za kutwa nchini humo kuanzia kesho Jumatatu, huku shule za bweni zikipewa hadi Jumatano kutekeleza agizo hilo. Aidha Vyuo Vikuu na taasisi za elimu za juu nchini humo zimetakiwa kufungwa kufikia Ijumaa ijayo.

Wasafiri wanaoingia Kenya watakiwa kujiweka karantini kwa siku 14

Hadi hivi sasa nchi zaidi ya 20 za Afrika zimethibitisha kukumbwa na Corona huku nchi za karibuni kabisa zikiwa ni pamoja na Ushelisheli, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kenya, Rwanda, Ethiopia, Sudan, Guinea na Mauritania.

Leo Jumapili pia, Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amesema, "ili kuzuia mripuko wa Corona hapa nchini, tumesimamisha safari za ndege zote za kuunganisha kwenda Ulaya kisiwani hapa kwa muda wa siku 30 ."