Wahajiri 400 wakamatwa wakijaribu kwenda Ulaya na kurejeshwa Libya
Shirika la Kimataifa la Wahajiri (IOM) limesema Gadi ya Pwani ya Libya imewakamata wahajiri 400 wakiwa safarini kuelekea Ulaya na kuwarejesha katika mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa liliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter jana Jumapili kuwa: Wahajiri 300 waliokuwa kwenye boti tatu za plastiki walikamatwa Jumamosi na kurejeshwa Tripoli. Wengine 105 walikamatwa jana Jumapili wakiwa kwenye boti mbili dhaifu za plastiki katika bahari ya Mediterania na kurejeshwa katika vituo vya kuhifadhi wakimbizi nchini Libya.
Safa Msehli, msemaji wa IOM amesema ni kitu kisichokubalika kuwarejesha katika 'kambi za mateso' nchini Libya wahajiri wenye mahitaji maalumu waliokuwa wakijaribu kuelekea Ulaya.
Hii ni katika hali ambayo, Serikali ya Muafaka wa Kitaifa ya Libya yenye makao yake mjini Tripoli imetangaza hali ya hatari kutokana na ugonjwa wa COVID-19 au Corona na kusema itafunga viwanja vyote vya ndege pamoja na bandari zote kuanzia leo Jumatatu. Hadi sasa hakuna kesi yoyote ya Corona iliyoripotiwa Libya, ambayo ni kitovu kikuu cha magendo ya wahajiri.
Mwaka jana wa 2019 maelfu yawahajiri ambao walikuwa na lengo la kuelekea nchi za Ulaya waliaga dunia katika bahari ya Mediterania.
Katika hatua nyingine, kundi la wahajiri 112 raia wa nchi za kaskazini mwa Afrika jana Jumapili waliokolewa wakizama baharini na kupelekwa katika kisiwa cha Malta. Wahajiri 1,500 wamewasili Malta tokea mwanzoni mwa mwaka huu hadi mapema Machi, ikilinganishwa na 3,400 waliowasili katika kisiwa hicho mwaka jana 2019.