Virusi vya Corona vyaendelea kusambaa kwa kasi barani Afrika
Somalia, Benin na Liberia ni nchi za hivi karibuni kabisa kuripoti kesi za ugonjwa wa Corona (Covid-19) barani Afrika, huku virusi hivyo vikiendelea kusambaa kwa kasi katika nchi za bara hilo.
Waziri wa Afya wa Somalia, Dakta Fauziya Abikar amesema aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huyo ni miongoni mwa watu wanne waliokuwa wamewekwa karantini mjini Mogadishu, baada ya kurejea nchini humo hivi karibuni wakitokea China.
Wakati huo huo, Wizara ya Habari ya Liberia imesema, muathirika wa ugonjwa huo ni Mkuu wa Wakala wa Mazingira wa nchi hiyo, ambaye alirejea nchini hivi karibuni akitokea Uswisi.
Jana Jumatatu pia, Waziri wa Afya wa Benin, Benjamin Hounkpatin alisema nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika ina kesi moja ya Corona, na muathiriwa ni raia wa Burkina Faso ambaye hivi karibuni aliitembelea Ubelgiji.
Kadhalika serikali ya Tanzania jana Jumatatu ilitangaza kuwepo mgonjwa wa Covid-19 ambaye aliingia nchini humo Jumapili akitokea Ubelgiji pia.
Kufikia sasa, nchi 30 kati ya 54 za Afrika zimekumbwa na virusi vya Corona, huku jitihada zikiendelea za kuzuia mripuko wa ugonjwa huo katika nchi ambazo hazijaathiriwa na vile vile kuzuia maambukizi zaidi katika nchi zilizoathiriwa.