Kundi la al-Shabaab laendelea kupata pigo nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59793-kundi_la_al_shabaab_laendelea_kupata_pigo_nchini_somalia
Jeshi la Somalia likishirikiana na askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (Amisom) limefanikiwa kuukomboa mji wa kistrataji wa Janale ulioko kwenye eneo la Lower Shabelle, kusini mwa Somalia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 17, 2020 04:29 UTC
  • Kundi la al-Shabaab laendelea kupata pigo nchini Somalia

Jeshi la Somalia likishirikiana na askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini humo (Amisom) limefanikiwa kuukomboa mji wa kistrataji wa Janale ulioko kwenye eneo la Lower Shabelle, kusini mwa Somalia.

Kamanda wa jeshi hilo Abdihamid Mohamed Dirir amesema operesheni za usalama za kukomboa miji muhimu kutoka kwenye makucha ya al-Shabaab zitaendelea.

Afisa huyo wa jeshi la Somalia ameeleza bayana kuwa, mji huo uliokombolewa uko katika sehemu ya kistrataji na ameahidi kukomboa maeneo yote yanayodhibitiwa na wapiganaji wa genge hilo la ukufurishaji.

Wanamgambo wa al-Shabaab

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Ijapokuwa mwaka 2011 genge hilo lilifurushwa kutoka kwenye miji mikubwa ya Somalia, lakini bado linadhibiti maeneo ya ndani ya vijijini ambako ni vigumu kufikiwa na wanajeshi wa serikali na wale wa kimataifa.