Corona yaua DRC na Mauritius, Algeria yafuta maandamano
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i59888-corona_yaua_drc_na_mauritius_algeria_yafuta_maandamano
Mgonjwa wa corona ameaga dunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hicho kikiwa ni kifo cha kwanza kilichosababishwa na ugonjwa huo nchini humo, huku kesi za maambukizi ya kirusi hicho barani Afrika zikiendelea kuongezeka.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2020 22:07 UTC
  • Corona yaua DRC na Mauritius, Algeria yafuta maandamano

Mgonjwa wa corona ameaga dunia katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hicho kikiwa ni kifo cha kwanza kilichosababishwa na ugonjwa huo nchini humo, huku kesi za maambukizi ya kirusi hicho barani Afrika zikiendelea kuongezeka.

Waziri wa Afya wa DRC, Eteni Longondo amethibitisha hayo katika ujumbe wake kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumamosi, sanjari na kutangaza kesi tano mpya za wagonjwa wa Covid-19 nchini humo.

Aidha jana Jumamosi, Mauritius ilisajili kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona nchini humo, huku idadi ya watu walioambukizwa kirusi hicho ikiongezeka na kufikia watu 13.

Nchini Algeria watu wasiopungua 12 wameaga dunia kutokana na corona na wengine karibu 100 wanasumbuliwa na virusi hivyo, jambo ambalo limepelekea kufutwa kwa maandamano ya kila wiki dhidi ya serikali kwa mara ya kwanza tokea Februari 2019, wakati aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika alipotangaza kuwa atagombea muhula wa tano wa urais.

Wataalamu wa afya duniani wanafanya jitihada za kutafuta chanjo ya corona

Kesi za maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 barani Afrika zimepita 800 hadi kufikia Ijumaa. 

Kwa mujibu wa taarifa aghalabu ya wagonjwa wa Covid-19 barani Afrika wametokea Ulaya na Marekani, na ili kuzuia ueneaji wa janga hili, nchi mbalimbali barani humo zimesimamisha safari za ndege kutoka nchi zilizokumbwa zaidi na janga hilo haswa nchi za Ulaya.