Ripoti: Mapigano ya kikoo yameua watu 70 Somalia
Kwa akali watu 70 wameuawa katika mizozo na mapigano ya kikoo nchini Somalia tokea Disemba mwaka jana 2019 hadi sasa.
Hayo ni kwa mujibu wa data zilizokusanywa na timu za waangailizi na maafisa wa serikali ambao wameonya kuwa, mizozo hiyo ya kikoo inarejesha nyuma jitihada za kurejesha amani, usalama na uthabiti katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Kwa mujibu wa ripoti, eneo la Lower Juba hususan magharibi mwa mji wa Kismayo linaongoza kwa migogoro hiyo ya kikoo, ambapo tokea Disemba 2019 hadi sasa watu wasiopungua 30 wameuawa.
Habari zaidi zinasema kuwa, katika mji wa Wanlawayn katika eneo la Lower Shabelle, watu 24 wameuawa pia katika mapigano ya kikoo.
Takwimu hizo za timu za waangailizi na maafisa wa serikali zinaonyesha kuwa, asilimia 90 ya watu zaidi ya 70 waliouawa katika mizozo hiyo ya kikoo nchini Somalia ni raia wasio na hatia.
Mizozo ya kikoo na kikabila inashuhudiwa nchini Somalia katika hali ambayo, taifa hilo la Pembe ya Afrika linakabiliwa na matatizo na majanga chungu nzima, ikiwemo njaa na mashambulizi ya kila uchao ya magenge ya kigaidi hasusan kundi la kitakfiri la al-Shabaab.