Maambukizi ya Corona Afrika; kuongezeka vifo na umaskini
Maambukizi ya maradhi ya corona barani Afrika yamezidisha wasiwasi kuhusu hali ya afya na matibabu na vile vile hali ya kiuchumi ya nchi mbalimbali za bara hilo. Katika uwanja huo, Kamisheni ya Kiuchumi ya Afrika yenye mfungamano na Umoja wa Mataifa imetahadharisha kuhusu uwezekano wa kuaga dunia zaidi ya watu 300,000 kutokana na maambukizi ya corona katika bara hilo.
Hata kama nchi mbalimbali za Kiafrika zimekumbwa na maambukizi ya virusi vya corona kwa kuchelewa kuliko maeneo mengine ya dunia lakini hivi sasa zaidi ya watu elfu 17 wameambukizwa corona na inatabiriwa kwamba Afrika itageuka kuwa kitovu cha maradhi ya Covid-19 iwapo maradhi hayo yataenea pakubwa barani humo. Algeria, Afrika Kusini, Misri, Morocco na Cameroon ni nchi za Kiafrika ambazo zina idadi kubwa ya kesi za maambukizi ya Covid-19 barani humo.
Bara la Afrika liko katika hatari ya kukumbwa na maambukizi makubwa ya corona katika hali ambayo kukosekana mfumo imara wa tiba, uhaba wa dawa na suhula za kutosha za kitiba, kushindwa idadi kubwa ya raia wa nchi za Kiafrika kupata huduma katika vituo vya afya na tiba, yote hayo yamezidisha wasiwasi kuhusu kuenea maambukizi ya virusi vya corona katika bara hilo. Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya jamii ya raia wa bara la Afrika wanaishi katika maeneo maskini na yale yasiyo rasmi; na ni asilimia 34 tu ya familia za Kiafrika ndizo zina uwezo wa kuosha mikono kwa maji na sabuni.
Profesa Dennis Mukwege mshindi wa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2017 ametadharisha kuhusu kuenea maambukizi ya virusi vya corona barani Afrika na kusisitiza kuwa: Bara la Afrika linakabiliwa na hatari kubwa kutokana na kutokuwa na miundomsingi madhubuti ya kiafya na kitiba. Kuwa mbaya hali ya kiuchumi katika akthari ya nchi za Afrka ni changamoto nyingine pia. Inatabiriwa kuwa ukuaji wa kiuchumi wa nchi za bara hilo unaweza kupungua kutoka asilimia 3.2 na kufikia asilimia 1.8; na hii ina maana kwamba karibu watu milioni 27 watakumbwa na umaskini wa moja kwa moja. Kwa mujibu wa matokeo ya utafiti uliofanywa na Umoja wa Afrika; kuenea ugonjwa wa Covid-19 kunaweza kusababisha kupotea ajira milioni 20 barani humo. Aidha sekta ya utalii barani Afrika itapata hasara ya zaidi ya dola bilioni 50.
Ahuna Eziakonwa Mkurugenzi wa Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa barani Afrika (UNDP) ametahadharisha kuwa: Kuenea virusi vya corona kutasambaratisha uchumi wa Afrika.
Takwimu zinaonyesha kuwa nchi 54 barani Afrika zimeathirika pakubwa mkabala na maambukizi ya virusi vya corona. Mapato ya akthari ya raia wa nchi hizo yanatokana na shughuli za utoaji huduma na zisizo za viwanda; na kuenea sasa maambukizi ya corona kumepelekea kufungwa shughuli zote au akthari yazo. Hali ya maisha ikiwemo idadi kubwa ya watu na umaskini katika aghalabu ya nchi za bara hilo vinakwamisha kutekelezwa kikamilifu sheria ya karantini; jambo ambalo litaathiri mustakbali wa uchumi na kijamii wa bara hilo. Kwa msingi huo inaonekana kuwa nchi za Kiafrika zinahitajia pakubwa misaada ya kimaada na uungaji mkono wa nchi tajiri na wa taasisi za kimataifa.
Kuchukuliwa hatua za kiuchumi ikiwemo kulipa madeni ya muda mrefu, kusamehe madeni, kusaidia ujenzi au kuboresha miundombinu ya kiuchumi ya nchi za Kiafrika na kutuma zana na suhula za afya na tiba pamoja na madawa ni miongoni mwa njia zitakazoweza kuzisaidia nchi za Kiafrika katika mapambano dhidi maambukizi ya virusi vya corona katika bara hilo.
Kristalina Giorgeva Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fedha Duniani (IMF) amewahutubu viongozi wa serikali, Umoja wa Mataifa na wawakilishi wengine kwamba: Afrika inakabiliwa na uhaba wa suhula na miundomsingi ya kitiba kwa ajili ya kukabiliana na janga hili la kitiba na afya; inahitajia dola zisizopungua bilioni 114 kwa ajili ya kukidhi haraka mahitaji yake ya kifedha.