Vifo vya corona vyaongezeka kwa asilimia 38 barani Afrika
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, vifo vinavyotokana na ugonjwa wa COVID-19 vimeongezeka kwa asilimia 38 barani Afrika.
Shirika hilo limetangaza habari hiyo kwenye ukurasa wake wa Twitter na kuongeza kuwa, maambukizi ya corona katika nchi za Afrika Kusini, Algeria, Cameroon, Ghana, Ivory Coast na Guinea ni makubwa zaidi ikilinganishwa na katika nchi nyingine za Afrika kiasi kwamba nchi hizo sita zinaunda asilimia 66 ya maambukizi yote ya corona yaliyoripotiwa Afrika hadi hivi sasa.
Daktari Matshidiso Moeti, mkurugenzi wa WHO barani Afrika amesema, hivi sasa kumeshathibitishwa kesi zaidi ya 23,000 za corona katika pembe mbalimbali za Afrika huku Afrika Kusini ikiwa inaongoza kwa maambukizi ikilinganishwa na nchi nyinginezo zote za bara hilo. Zaidi ya watu elfu tatu na 953 wameshathibitishwa kukumbwa na corona hadi hivi sasa nchini Afrika Kusini.
Daktari Moeti ameongeza kuwa, katika baadhi ya nchi za magharibi mwa Afrika pamoja na katika nchi kama Tanzania, kuna wasiwasi wa kuongezeka zaidi maambukizi ya ugonjwa huo.
Mkurugenzi huyo wa Shirika la Afya Duniani barani Afrika amesisitiza pia kuwa, shirika hilo limetiwa wasiwasi na uwezo mdogo wa wananchi wa bara la Afrika wa kupata huduma zinazotakiwa za kupambana na corona.