Polisi Uganda: Maandamano ya upinzani hayana kibali
Polisi ya Uganda imeonya wafuasi wa upinzani nchini humo dhidi ya kushiriki maandamano ya Mei 5 na kusisitiza kuwa maandamano hayo hayajapata ridhaa ya serikali.
Msemaji wa Polisi jijini Kampala, Patrick Onyango amesema kuwa ombi la Dakta Kizza Besigye, kinara wa chama cha FDC la kufanyika maandamano hayo jijini Kampala halijakidhi masharti ya idara ya polisi na kwa msingi huo, maandamano hayo ni batili.
Amesema polisi itakabiliana na yeyote atakayeshiriki maandamano hayo yaliyotajwa kuwa haramu.
Aprili 25, Kanali Besigye aliliandikia barua jeshi la polisi la nchi hiyo ya Afrika Mashariki, kulijulisha juu ya maandamano ya wafuasi wa chama chake mnao Mei 5 kuanzia kijiji cha Najjanankumbi ambapo kuna makao makuu ya chama hicho hadi shule ya msingi ya Nakivubo Blue.
Jumanne iliyopita, kiongozi wa ngazi ya juu wa chama cha FDC Ibrahim Ssemujju Nganda alisema kuwa, maandamano yaliyoitishwa kwa ajili ya kupinga mwenendo wa kuhesabu kura za uchaguzi mkuu uliopita nchini Uganda, yapo pale pale.
Mgogoro wa kisiasa nchini Uganda uliibuka baada ya mirengo ya upinzani kupinga matokeo yaliyompa ushindi Rais Yoweri Kaguta Museveni wa nchi hiyo katika uchaguzi uliofanyika mwezi Februari mwaka huu.