Rais Rajoelina awaponda Wamagharibi kwa kuwadhalilisha wanasayansi wa Kiafrika
Rais Andry Rajoelina wa Madagascar amezikosoa vikali nchi za Ulaya kwa kutilia shaka dawa ya asili inayodaiwa kutibu ugonjwa wa Covid-19 iliyozinduliwa na nchi yake akisisitiza kuwa, iwapo dawa hiyo ingelikuwa imegunduliwa katika nchi za Ulaya, isingetiliwa shaka.
Rais Rajaoleina amesema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya France 24 ya Ufaransa na kueleza bayana kuwa, "wanasayansi wa Kiafrika hawapaswi kudhalilishwa na kuonwa duni."
Rais huyo wa Madagascar amehoji, "iwapo ni nchi ya Ulaya ingeligundua dawa hii, kungekuwa na shaka kiasi hiki? Sidhani!"
Shirika la Afya Duniani sambamba na kutahadharisha juu ya matumizi ya dawa hiyo inayofahamika kama Covid Organics, liliwataka viongozi wa serikali ya Antananarivo kuifanyia utafiti wa kitiba.
Aidha Umoja wa Afrika umeitaka Madagascar kuweka wazi matokeo ya uchunguzi wa kitaalamu kuhusiana na taathira na usalama wa dawa hiyo.
Hata hivyo, nchi za Afrika zikiwemo Niger, Equatorial Guinea, Senegal, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tanzania tayari zimekwishaagiza dawa hiyo kwa ajili ya kuifanyia utafiti. Licha ya Madagascar kusajili kesi 193 za waathirika wa virusi vya Corona, lakini hakuna mtu yeyote nchini humo aliyethibitishwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa Covid-19.