May 14, 2020 11:08 UTC
  • Jeshi la Nigeria lawakomboa raia 72 waliokuwa wakishikiliwa mateka na Boko Haram

Jeshi la Nigeria limefanikiwa kuwakomboa raia 72 waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi la kigaidi la Boko Haram katika jimbo la Borno.

Kanali Musa Sagir, msemaji wa jeshi la Nigeria amesema kuwa, raia hao wamekombolewa kufuatia operesheni kali ya jeshi iliyofanywa dhidi ya ngome za wanamgambo wa Boko Haram katika moja ya vijiji vya jimbo la Borno lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Aidha amesema, idadi kubwa ya wanachama wa kundi hilo wamekimbia huku jeshi la Nigeria likifanikiwa kukamata silaha nyingi. Inaelezwa kuwa, wanajeshi wawili wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika operesheni hiyo.

Msemaji huyo wa jeshi la Nigeria ameongeza kuwa, waliokombolewa katika operesheni hiyo ya kijeshi ni wanawake 34 na watoto 38 na kwamba, wanachama 18 wa kundi hilo la kigaidi wameuawa.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram lilianzisha shughuli zake za kigaidi mwaka 2009 kaskazini mwa Nigeria ambapo hadi sasa limepanua wigo wake hadi katika nchi za Niger, Cameroon na kaskazini mwa Chad.

Kwa mujibu wa ripoti za Umoja wa Mataifa, katika muongo mmoja wa shughuli za kundi la Boko Haram nchini Nigeria, zaidi ya watu elfu 30 wameuawa na wengine wanaokaribia milioni tatu wamekuwa wakimbizi.

Serikali ya Nigeria inayoongozwa na Rais Muhamadu Buhari imeendelea kulaumiwa na kukosolewa kutokana na kuzembea katika kukakabiliana na kundi hilo la kigaidi ambalo limevuruga usalama wa nchi hiyo na nchi za jirani.

Tags